Marekani itaunga mkono makubaliano ya tabia nchi?
1 Juni 2017Usiku wa kuamkia Jumatano Trump aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba atatoa tangazo hilo Alhamis, baada ya washirika wa nchi hiyo kote ulimwenguni kuonya kuhusiana na yanayoweza kuikabili Marekani iwapo itajiondoa. Rais huyo lakini amemuweka kila mmoja katika hali ya kutofahamu litakalotokea kwani anasema bado anasikiliza maoni ya watu wengi kutoka kila upande.
Ikulu ya Marekani iliashiria kwamba upo uwezekano wa Trump kujiondoa kutoka kwenye makubaliano hayo na atimize mojawapo ya ahadi kuu alizozitoa wakati wa kampeni.
Kila mmoja ameonya kwamba hakuna uamuzi ambao ni wa mwisho hadi pale Trump atakapoutangaza. Rais huyo anajulikana kwa kuwa na tabia ya kubadilisha fikra zake katika maamuzi makubwa na kutafuta ushauri kutoka nje na ndani ya utawala wake, huku wengi wakiwa na maoni tofauti na yeye mwenyewe afanye uamuzi katika dakika ya mwisho.
China yasema itasalia kuunga mkono makubaliano hayo
Uingereza kupitia waziri wa mambo ya nje Boris Johnson, inaitaka Marekani kuwa mstari wa mbele katika kuyashughulikia masuala ya tabia nchi.
"Naendelea kuishinikiza Marekani katika kila ngazi kuendelea kuchukulia tabia nchi kwa umuhimu mkubwa na kuonesha uongozi ambao Marekani imeonesha katika miaka ya nyuma," alisema Boris Johnson.
China nayo ilisema Alhamis kwamba itaendelea kuyaunga mkono makubaliano hayo ya Paris. Katika kikao chake na waandishi wa habari cha kila siku, waziri wa mambo ya nje wa China Hua Chunying, alisema makubaliano hayo hayakuafikiwa kwa urahisi na yanawakilisha makubaliano makubwa ya jamii ya kimataifa.
"Tabia nchi ni mabadiliko ya dunia nzima, hakuna nchi inayoweza kujiondoa kutoka kwenye jambo hili," alisema Chunying.
Makubaliano ya Paris yalitiwa saini na mataifa 195
Kiongozi mkuu wa Marekani katika makubaliano hayo ya Paris ya mwaka 2015, Todd Stern, alimuonya Trump kwamba kujiondoa ni jambo litakalokuwa na athari katika uongozi wake.
"Nafikiri iwapo rais ataiondoa Marekani katika yale makubaliano ya Paris na kujiunga na Syria na Nicaragua kama nchi nyengine mbili za pekee dunia nzima zilizo nje ya makubaliano hayo, nafikiri litakuwa ni jambo litakaloutia doa uongozi wake," alisema Stern.
Makubaliano hayo ya Paris yalitiwa saini na mataifa 195 na iwapo Marekani itajiondoa basi itajitenga na washirika wake wengi waliojadiliana kwa miaka mingi na kuafikiana kuhusiana na kupunguza utoaji wa gesi ya kaboni.
Alipokuwa katika ziara yake ya Ulaya wiki iliyopita, viongozi wa Ulaya na hata kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis walimtaka Trump, asiiondoe nchi yake katika makubaliano hayo.
Mwandishi: Jacob Safari/APE/Reuters
Mhariri: Josephat Charo