Marekani itayari kuzungumza na Korea Kaskazini
13 Desemba 2017Tillerson lakini amesisitiza wanadhamiria kuishinikiza nchi hiyo kuachana na mpango wake wa nyuklia.
China na Urusi zimelipokea vyema tamko hilo la Tillerson licha ya Ikulu ya Rais wa Marekani kuonekana kutilia shaka mtizamo huo baada ya kutoa taarifa kuwa mtizamo wa Rais Donald Trump kuihusu Korea Kaskazini haujabadilika.
Licha ya kuwa msemaji wa Ikulu ya Rais wa Marekani - White House, Sarah Sanders kutosema moja kwa moja maoni ya Trump ni yapi, Rais huyo katika kipindi cha nyuma amenukuliwa akisema Waziri wake wa mambo ya nje anapoteza muda kufanya mazungumzo na Korea Kaskazini.
Kremlin inafurahishwa na matamshi ya tija ya Tillerson
Nchini China, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Lu Kang, amesema China ina matumaini kuwa Marekani na Korea Kaskazini zitachukua hatua za tija kuelekea mazungumzo ya moja kwa moja yatakayopunguza mzozo katika rasi ya Korea.
Nchini Urusi, msemaji wa Ikulu ya Rais ya Kremlin Dmitry Peskov amewaambia wanahabari kuwa matamshi ya tija kama aliyoyatoa Tillerson yanawafurahisha zaidi kuliko cheche za maneno na vitisho ambavyo wamekuwa wakisikia hadi sasa, na mtizamo huo mpya wa Marekani unapokelewa vyema.
Huku Tillerson akisisitiza umuhimu wa kuwepo mazungumzo kati ya nchi yake na Korea Kaskazini ili kuutatua mzozo wa kinyuklia, kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ameapa kulifanya taifa lake lenye nguvu zaidi kinyuklia na kijeshi duniani.
Trump ameahidi kuwa Kim hataruhusiwa kufanikisha malengo yake ya kuunda silaha za kinyuklia zilizo na uwezo wa kushambulia Marekani. Marekani imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza juhudi za kidiplomasia za kuitenga Korea Kaskazini na kuukwamisha uchumi wa taifa hilo kupitia vikwazo.
Maafisa wa Korea kaskazini hawakuonesha kuwa tayari kwa mazungumzo
Hapo jana katika hafla mbili tofauti, Trump alionya kuwa juhudi hizo za kuiadhibu Korea Kaskazini zitaendelea hadi pale bomu la kwanza litakapodondoshwa. Hata hivyo amesema milango ya mazungumzo na Korea Kaskazini iko wazi zaidi wakati huu kuliko kipindi cha nyuma, akilegeza msimamo wake mkali aliokuwa nao kuhusu nchi hiyo.
Jeffrey Feltman mkuu wa masuala ya kisiasa wa umoja wa Mataifa ambaye ameizuru Korea Kaskazini hivi karibuni amesema maafisa wa nchi hiyo wamemueleza kuwa ni muhimu kuepusha vita lakini hawakupendekeza bayana kuwa tayari kwa mazungumzo.
Mwishoni mwa juma lililopita, Feltman alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini Ri Yong- Ho na naibu wake Pak Myong Kuk katika ziara hiyo ya kwanza kufanywa na afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa nchini humo tangu mwaka 2011.
Mwandishi: Caro Robi/afp
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman