1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuendelea na matumizi ya chanjo ya J&J

Sylvia Mwehozi
24 Aprili 2021

Maafisa wa afya wa Marekani wameamua kuondoa zuio la siku 11 dhidi ya matumizi ya chanjo ya Johnson & Johnson baada ya wanasayansi kuhitimisha kuwa faida zake ni kubwa ukilinganisha na tatizo la damu kuganda

https://p.dw.com/p/3sVdj
Weltspiegel 14.04.2021 | Corona | Impfstoff Johnson & Johnson
Picha: Dado Ruvic/REUTERS

Mamlaka ya udhibiti wa chakula na madawa ya Marekani ilitoa idhini ya kuendelea na chanjo ya J&J ambayo inatolewa kwa dozi moja ikisema ilikuwa na ufanisi mkubwa katika kupambana na COVID-19 na kwamba changamoto ya damu kuganda inaweza kushughulikiwa.

Serikali ilibaini kuwa watu 15 kati ya karibu milioni 8 waliopatiwa chanjo hiyo walionyesha dalili ya damu kuganda. Wote walikuwa ni wanawake chini ya umri wa miaka 50 ambapo watatu walifariki na wengine wangali bado hospitali. Umoja wa Ulaya mapema wiki hii nao ulitangaza kuendelea na matumizi ya chanjo ya J&J.

Na Hospitali nchini India zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vifaa vya kupumilia kwa wagonjwa wa Covid-19 wakati maambukizi ya maradhi hayo yakizidi kuongezeka.

SIku ya Ijumaa India ilitangaza maambukizi mapya zaidi ya 330,000 na vifo 2000 ndani ya siku moja ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa duniani.

Idadi hiyo imepandisha visa vya Covid-19 nchini India kufikia karibu milioni 16 na kuwa taifa la pili duniani baada ya Marekani kuwa na kiwango cha juu cha maradhi hayo.

Umoja wa Falme za Kiarabu na Canada ni miongoni mwa mataifa yaliyozuia ndege zote kutoka India. Wakati huohuo moto uliozuka jana kwenye hospitali moja magharibi mwa India ulisababisha vifo vya watu 13 waliokuwa wamelazwa kwenye wodi ya wagonjwa wa COVID 19.