Marekani yatangaza msaada mpya wa dola milioni 160 kwa Haiti
26 Septemba 2024Msaada huo umetangazwa Jumatano wakati Waziri Mkuu wa Haiti Garry Conille akisema taifa hilo bado lina safari ndefu kuvishinda vita dhidi ya makundi ya wahalifu wanaodhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu, Port-au-Prince.
Waziri wa mambo ya Kigeni wa Marekani Anthony Blinken aliyewahi kufanya ziara Port-au-Prince mapema mwezi huu alitangaza msaada huo mpya kwa Haiti wakati wa mkutano wa pembezoni wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na mawaziri kuhusu hali nchini Haiti.
Soma zaidi: Marekani yatoa wito wa kuhuisha kikosi cha usalama Haiti
Blinken alisema, "Leo ninaweza kutangaza kuwa tunaongeza msaada wa dola za Kimarekani milioni 160, kulisaidia jeshi la polisi la Haiti, kuwekeza katika kuzuia machafuko na kuanza kazi ya kuiimarisha na kuirejesha Haiti katika hali ya kawaidi. Natangaza pia vikwazo vya ziada kwa wale wanaotaka kuzidhoofisha taasisi za Haiti na kuwatisha watu wake ili kuhamasisha uwajibikaji. "
Msaada huo unafanya jumla ya fedha zilizoahidiwa na Marekani tangu mwaka 2021 kwa ajili ya taifa hilo kufikia dola za Kimarekani bilioni 1.3. Licha ya kutangazwa kwa msaada huo, Waziri Mkuu wa mpito wa Haiti Garry Conille amesema taifa hilo bado lina safari ndefu katika kuvishinda vita dhidi ya makundi ya wahalifu. Conille ameyasema hayo wakati muda uliowekwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kulisaidia taifa hilo ukikaribia kumalizika.
Haiti inakabiliwa na mgogoro unaotokana na mashambulizi ya magenge ya wahalifu katika bandari kuu kwenye mji mkuu Port au Prince. Bandari hiyo ndiyo kituo muhimu cha kuingizia misaada na bidhaa nchini humo.
Meli katika bandari za Haiti zaendelea kushambuliwa
Mapema wiki hii mmoja wa maafisa wa usafirishaji bidhaa kwa njia ya meli aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa, meli zimekuwa zikirushiwa risasi kwa madhumuni ya kuzizuia zisitie nanga na kupakua mizigo kutoka kwenye makontena.
Bandari kubwa za Haiti na Uwanja wa ndege wa Kimataifa vilifungwa kwa karibu miezi mitatu mwaka huu baada ya machafuko kupamba moto mwishoni mwa mwezi Februari.
Soma zaidi: Kenya yaongeza maafisa 200 zaidi nchini Haiti
Machafuko hayo yalihusisha kutoroka kwa wafungwa gerezani na aliyekuwa Waziri Mkuu Ariel Henry alijiuzulu. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, idadi ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na machafuko hayo sasa ni zaidi ya watu 700,000
Takriban mataifa 10 yaliahidi kupeleka wanajeshi 3,100 kusaidia kurejesha utulivu nchini humo, lakini hadi sasa ni wanajeshi 400 pekee waliopelekwa. Kenya taifa linaloongaza ujumbe wa kulinda amani kupitia Waziri Kiongozi Musalia Mudavadi, ilisema kuwa ufadhili kwa ajili ya kukimu wanajeshi waliopelekwa Haiti hautoshi. Ametoa wito kwa nchi zilizotoa ahadi ya kupeleka wanajeshi kuongeza kasi ili zitimize ahadi hiyo.