Marekani kuisaidia Tanzania kiusalama
25 Julai 2024Hayo yameelezwa na Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayehusika na masuala ya siasa, John Bass aliyekamilisha ziara yake ya siku tatu katika nchi za Chad na Tanzania.
Licha ya kutotaja ni mashirikiano yenye msaada wa aina gani katika eneo la usalama, waziri huyo amesema ni shabaha ya Marekani kudumisha ushirikiano na Tanzania ikiwamo kuimarisha sekta ya usalama.
Mojawapo ya nchi zilizopeleka vikosi vyake Msumbiji
Amesema katika majadiliano yake na viongozi wa kiserikali, miongoni mwa mambo yaliyotizamwa ni kuona kwamba kwa kiasi gani Marekani itakavyoendelea kuwa karibu na Tanzania kusaidia usalama katika eneo lake la kusini.
"Nadhani katika fursa tulizonazo ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wetu wa kiusalama kuisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto za kigaidi katika mpaka wake wa kusini," alisema Bass.
Tanzania ambayo katika upande wake wa kusini inapakana na jirani yake Msumbiji ni sehemu ya mataifa machache yaliyopeleka vikosi vyake nchini humo kwa ajili ya kuwakabili magaidi wenye mafungamano na kundi la al-Qaeda.
Akiwa nchini hivi karibuni, Rais wa Msumbiji taifa ambalo linajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwezi mmoja ujao, Filipe Nyusi alisifu juhudi za vikosi vya Sadc kufanikisha kuwafurusha waasi hao.
Alipoulizwa na DW kupata maoni yake kama Marekani imechelewa kutoa uhakikisho kuhusu suala la usalama katika eneo la kusini hasa katika wakati huu ambako hali ya usalama imeanza kutengamaa, mchambuzi wa masuala ya kimataifa kutoka chuo cha diplomasia, Denis Konga, alikuwa na haya ya kusema.
"Suala la usalama ni muhimu mno ila Marekani haiathiriki sana na matukio ya Afrika. Kwa hiyo kwa ahadi hii ya kushirikiana na Tanzania, hii italeta usalama sio tu kwa Tanzania bali kwa washirika wake pia katika kanda hiyo," alisema Konga.
Marekani kuwakaribisha Wasudan
Ama mwanadiplomasia huyo, amesema Marekani itaongeza ushirika wake kwa ajili ya kuimarisha sekta ya afya ili kuwezesha huduma za kukabiliana na maambukizi ya HIV na Malaria.
Alipoulizwa huhusu suala la uchaguzi hasa wakati huu ambako Tanzania imeanza mchaka mchaka kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, alisema ni muhimu uchaguzi ukafanyik katika mazingira ya uwazi na ukweli na kusisitiza kuwa wahusika wanapaswa kuheshimu maamuzi yanayofanywa na wananchi kupitia sanduku la kura.
Katika duru nyingine, Bass amesema Marekani na jumuiya nyingine ya kimataifa ina wajibu wa kunyosha mkono kuwasitiri na kuwakaribisha wananchi wa Sudan wanaokimbia mapigano huku akiitolea mkono wa heko chad kwa namna inavyopaswa kuwakaribisha wakimbizi.
Mwishoni wa ziara yake jijini Dar es salaam mwanadiplomasia huyo mbali ya kusisitiza namna taifa lake linavyoipa kipaumbele sekta ya afya, amesema ni msingi wa Marekani kudumisha mashirikiano yanayozingatia maslahi ya pande zote.