Marekani kujiondoa rasmi makubaliano ya tabia nchi ya Paris
5 Novemba 2019Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa mpinzani mkubwa wa makubaliano hayo wakati alipokuwa anawania kiti cha urais, na utawala wake umekuwa ukifanya kila unaloliweza kubadilisha sheria za mazingira, ukisema zinazuwia biashara na kutoa kwa nchi nyingine nguvu ya ushindani.
Pompeo alielezea kuhusu kile alichokiita "mzigo usio wa haki wa kiuchumi uliowekwa kwa wafanyakazi wa Marekani, biashara, na walipa kodi, kwa ahadi za Marekani zilizotolewa chini ya makubaliano hayo," wakati akitangaza kujitoa huko. Amesema ,"mfano bora na wenye uhalisia" utapendekezwa na Marekani kupinga makubaliano hayo ya dunia.
Makubaliano ya mwaka 2015 yalitiwa saini na karibu nchi zote, na kuuweka utawala wa Trump dhidi ya karibu washirika wake wote pamoja na washindani wake wakuu kuhusiana na suala la mabadiliko ya tabia nchi. Trump binafsi ni mtu mwenye shaka na mabadiliko ya tabia nchi.
Utawala wa Trump rasmi uliuarifu Umoja wa mataifa hatua yake hiyo ya kujitoa siku ya Jumatatu, ukianza mchakato wa mwaka mmoja ambao utakamilika siku moja baada ya uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2020.
Msemaji wa Umoja wa mataifa alilithibitishia shirika la habari la Ujerumani dpa kuwa taasisi hiyo ya dunia imepokea barua ya Marekani.
Trump kwa kawaida hutumia hotuba katika mikutano yake ya kisiasa kuonesha mapenzi yake kwa hewa safi na maji safi na salama. "Tuna hewa safi kabisa katika dunia hapa Marekani," ni neno linalojirudia kila mara kutoka kwa rais.
Hata hivyo , uchunguzi umeonya kuwa tangu mwaka 2016 baadhi ya aina ya uchafuzi wa hewa unaongezeka.
Duniani, wanasayansi kwa jumla wana wasi wasi kuwa ongezeko la joto unaosababishwa na utoaji wa gesi chafu wa binadamu utasababisha hali mbaya kwa maisha katika sayari hii.
Ufaransa wakati huo huo imelalamikia uamuzi huo wa Marekani kuuarifu rasmi Umoja wa mataifa kuwa inajitoa kutoka mkataba huo wa paris. Wakati hatua hiyo ilikuwa ikitarajiwa ,"tunasikitika na inaufanya ushirika wa Ufaransa na China kuhusu mazingira na bio anuai kuwa muhimu zaidi", ofisi ya rais wa Ufaransa amesema wakati rais Emmanuel Macron akiwa katika ziara rasmi nchini China.
rtre / afpe / dpae