1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kupeleka vikosi vya kijeshi nchini Saudi Arabia.

21 Septemba 2019

Rais Donald Trump ameidhinisha hatua ya kupeleka vikosi zaidi vya kijeshi Saudi Arabia kusaidia vikosi vya ulinzi vya angani nchini humo. Hii ni baada ya shambulizi lililoharibu viwanda vikuu vya mafuta nchini humo.

https://p.dw.com/p/3PzWf
Saudi-Arabien Nach Angriff auf Ölanlagen |
Picha: picture-alliance/dpa/A. Nabil

Waziri wa ulinzi wa Marekani Mark Esper amethibitisha hatua hiyo ya kupelekwa kwa vikosi hivyo zaidi vya kijeshi nchini Saudi Arabia jana Ijumaa. Idadi kamili ya maafisa wa kijeshi na vifaa vitakavyotumiwa bado haijabainika lakini itakuwa sehemu ya "uhamishaji wa wastani'' katika eneo hilo. Hii ni kulingana na jenerali wa jeshi la wanamaji Joseph Dunford, ambaye ni mwenyekiti wa kundi shirikishi la wakuu wa kijeshi.

"Kwa kujibu ombi la taifa hilo la kifalme, rais ameidhinisha kupelekwa kwa vikosi vya kijeshi vya Marekani ambavyo vitatekeleza jukumu la ulinzi  na kuangazia zaidi ulinzi wa angani na makombora," Esper aliwaambia wanahabari.

Tangazo hilo linajiri baada ya shambulizi la Sepetmba 14 dhidi ya muundo msingi mkuu wa mafuta nchini Saudi Arabia ambalo lilitatiza nusu ya usambazaji wa bidhaa ya mafuta nchini humo. Waasi wa kihouthi nchini Yemen wamedai kuhusika katika shambulizi hilo lakini Marekani na Saudi Arabia zinashuku kuwa Iran ndio iliyohusika. Iran inayoungwa mkono na kundi hilo la kihouthi, imekanusha madai hayo.

Mapema jana Ijumaa, waasi wa kihuothi nchini Yemen walisema kuwa wanasitisha mashambulizi yanayotekelezwa na ndege zisizokuwa na marubani nchini Saudi Arabia. Mahdi al-Mashat, kiongozi wa baraza kuu la kisiasa la kihouthi, amesema kuwa ana matumaini " hatua hiyo itapokelewa vyema na Saudi Arabia".

Aliongeza kuwa kundi hilo linasubiri majibu yakuridhisha kutoka Saudi Arabia .

Al-Mashat amesema kuwa lengo kuu la mpango huo wa amani ni " kuokoa damu ya raia wa Yemen na kupata msamaha,"  na kuongeza kuwa " kuzingatia vita sio matamanio ya mtu yeyote"

Al-Mashat pia alitoa wito wa kufunguliwa kwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sanaa ili kufikia bandari ya Hodeida.

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umekuwa ukitekeleza mashambulizi dhidi ya waasi wa kihouthi nchini Yemen tangu mwaka 2015. Maelfu ya watu wamefariki katika mapigano hayo na Umoja wa Mataifa umeyataja kuwa mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.