Marekani kutuma ujumbe usio rasmi Taiwan baada ya uchaguzi
11 Januari 2024Marekani inakusudia kutuma ujumbe usio rasmi huko Taiwan baada ya uchaguzi muhimu katika kisiwa hicho kinachojitawala na kuionya China dhidi ya uchokozi wowote wa kijeshi. Hatua hiyo ya Washington inajiri huku kukiwa na mvutano unaozidi kuongezeka kuhusu uchaguzi wa Jumamosi.
Afisa mmoja mwandamizi katika utawala wa Rais Joe Biden, aliyezungumza na waandishi wa habari kwa sharti la kutotajwa jina, alisema Washington haiungi mkono upande wowote katika uchaguzi huo.
Fahamu wagombea wa Taiwan: Wagombea Urais Taiwan wachuana katika mdahalo kabla ya uchaguzi
Washington imeionya China dhidi ya kuzusha mvutano katika uchaguzi huo, ambao unatazamwa kwa karibu katika kuamua mustakabali wa uhusiano wa Taiwan na Beijing.
China imeapa kwamba haitakubali kamwe kuachana na dhamira yake ya kukitwaa kisiwa hicho siku moja. Taiwan itafanya uchaguzi wa rais na bunge siku ya Jumamosi, katikati mwa mivutano ya siasa za kikanda.