Marekani kuwasaidia wanaojisaidia kupambana na Ukimwi
19 Septemba 2017Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson, amebainisha vipaumbele vya mpango wa dharura wa rais kwa ajili ya msaada wa masuala ya Ukimwi (PEPFAR), ambao ni mhimili wa msaada wa Marekani kwa sekta ya afya unaosaidia matibabu ya Virusi vya Ukimwi (VVU), upimaji na ushauri kwa mamilioni ya watu duniani.
Utawala wa Rais Donald Trump umeomba fedha za mpango huo zipunguzwe kwa dola bilioni moja mwaka huu, lakini kamati ya baraza la Seneti ilipiga kura wiki iliyopita kutobadilisha ufadhili ambao kwa kawaida ni wa dola bilioni 6.
"Serikali ya Donald Trump ina nia ya kujibu masuala ya Ukimwi duniani na kuonyesha wazi namna kila dola ya Marekani inavyotumika ," alisema Tillerson katika ripoti yake.
Hata hivyo, serikali hiyo ya Marekani haikuweka wazi ni mipango gani utakaopungzwa, lakini wizara ya mambo ya nje inasisitiza kwamba itaendelea kutoa matibabu kwa watu wanaoendelea kuyapokea.
PEPFAR itaendela na mipango yake ndani ya nchi zaidi ya 50. Lakini kwa kuongeza athari yake itaweka nguvu zake katika mataifa 13 ambayo yanaelekea kuudhibiti ugonjwa huo kwa maana ya kwamba kunakuwepo na vifo vingi kila mwaka vinavyotokana na Ukimwi kuliko maambukizi mapya ya VVU.
Mataifa hayo yanajumuisha Kenya, Zambia, Tanzania, Uganda, Zimbabwe, Malawi, Lesotho, Ivory Coast, Botswana, Namibia, Swaziland, Haiti na Rwanda.
Kwa upande wake, Balozi Deborah Birx, mratibu wa Marekani kuhusu Ukimwi duniani, anasema wameamua kushughulika na mataifa ambayo kwa pamoja wanaweza kufikia mafanikio wakishirikiana na jamii pamoja na serikali.
Aidha kazi hii itafanywa kwa ushirikiano na mfuko wa ufadhili duniani wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria na Shirika la UNAIDS miongoni mwa mashirika mengine.
Nchi tano kati ya nchi zilizolengwa - Lesotho, Swaziland, Malawi, Zambia na Zimbabwe - zipo mstari wa mbele kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi kutokana na utafiti wa kudhibiti na kuzuwiya magonjwa wa Chuo Kikuu cha Colombia, serikali na washirika wa mashirika yasio ya kiserikali.
Awali mwezi Mei, wabunge wa Republican waliufokea utawala wa Trump kwa kupendekeza bajeti ya dola bilioni 5 kwa PEPFAR iliyopunguzwa takriban dola bilioni moja kutoka kwa bajeti ya hivi karibuni ya dola bilioni 6.
Wakfu wa Bill na Melinda Gates wiki iliyopita ulionya kupungua kidogo kwa ufadhili wa masuala ya Ukimwi kunaweza kuzuwia faida kubwa katika kudhibiti ugonjwa huo.
"Katika miaka mitano hadi sita iliyopita, maraisi wa Marekani wamependekeza kupunguzwa bajeti ya PEPFAR lakini bunge linalodhibiti bajeti limerejesha upya bajeti hiyo," anasema Balozi Birx.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman