1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Marekani: Mripuko wa mabomba ya Nord Stream ilikua hujuma

8 Machi 2023

Taarifa za kijasusi zilizotolewa na maafisa wa Marekani zinaonyesha kwamba kundi moja linaloiunga mkono Ukraine, ndilo lililofanya hujuma katika mabomba ya gesi ya chini ya maji ya Nord Stream.

https://p.dw.com/p/4ONNE
Pressebild Nord Stream 2
Picha: Nikolai Ryutin/Nord Stream 2

Mabomba hayo yanatoka Urusi kuelekea Ulaya na tukio hilo lilifanyika Septemba mwaka jana, ila hakukuwa na ushahidi wa serikali ya Ukraine kuhusika. Haya ni kwa mujibu wa gazeti la New York Times.

Mripuko wa mabomba hayo ya chini ya maji miezi saba baada ya Urusi kuanza uvamizi wake nchini Ukraine ulitokea katika eneo la kiuchumi la Sweden na Denmark katika bahari ya Baltic. Nchi zote mbili zimesema kwamba miripuko hiyo ilifanywa kusudi ila hawajamuweka wazi mhusika.

Marekani na Jumuiya ya Kujihami ya NATO wameyataja mashambulizi katika mabomba hayo kama "kitendo cha hujuma" huku Urusi ikizilaumu nchi za Magharibi na kutaka uchunguzi huru ufanyike. Hakuna upande uliotoa ushahidi wa aina yoyote.

Schweden Archivbild Leck Nord Stream
Gasi ikivuja kutoka kwenye bomba la Nord Stream lililo baharini SwedenPicha: Swedish Coast Guard Handout/Anadolu Agency/picture alliance

Marekani kuwa na imani na uchunguzi wa nchi husika

Ripoti hiyo ya gazeti la New York Times imewanukuu maafisa wa Marekani wakisema hakuna ushahidi kwamba Rais Volodymyr Zelenskiy au wasaidizi wake wakuu walihusika au wahusika walikuwa wanafanya kitendo hicho kwa masharti ya afisa yeyote wa serikali ya Ukraine. Hakuna kundi lolote linaloiunga mkono Ukraine lililotajwa kuhusika na tukio hilo.

Katika taarifa msaidizi wa Rais Zelenskiy, Mykhailo Podolyak amesema haiingii akilini na kwamba ni wazi kuwa Ukraine haikuhusika. Marekani kupitia kwa msemaji wa ikulu ya White House, Ned Price, imesema inasubiri uchunguzi unaofanywa na Ujerumani, Sweden na Denmark.

"Tuna imani kamili katika uchunguzi wanaoufanya, bila shaka tutasubiri uchunguzi huo ukamilike na tuone watakachokisema. Ila kwa mara nyengin e tuna imani na washirika wetu wa Ulaya wanaofanya uchunguzi huu," alisema Price.

Hayo yakiarifiwa naibu msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Farhan Haq, amewaambia waandishi wa habari kwamba mkuu huyo Umoja wa Mataifa amewasili Ukraine kukutana na Rais Volodymyr Zelenskiy katika ziara yake ya tatu nchini humo tangu Urusi ifanye uvamizi wake.

Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa na viongozi hao wawili mwendelezo wa mpango wa usafirishaji wa nafaka katika Bahari Nyeusi pamoja na masuala mengine muhimu. Hakuna taarifa zaidi iliyotolewa kuhusiana na ziara hiyo.

New York | UN-Generalsekretär Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Manuel E./Xinhua News Agency/picture alliance

Ukraine yaendelea kuupigania mji wa Bakhmut

Ama katika uwanja wa mapambano, vikosi vya Ukraine vimeendelea kuupigania mji wa mashariki wa Bakhmut licha ya majeshi ya Urusi na mamluki kuwazingira. Rais Zelenskiy amerudia ujumbe wake kwamba kuyateka tena maeneo yaliyokaliwa ndilo lengo lake kuu.

Taarifa iliyotolewa na mamlaka ya jeshi la Ukraine usiku wa kuamkia Jumatano imesema, jeshi la nchi hiyo limezuia mashambulizi yaliyokuwa yanaulenga mji wa Bakhmut na Ivanivske upande wa mashariki na upande wa magharibi katika mji wa Klishchiivka.

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema kutekwa kwa Bakhmut ni muhimu katika kuudhoofisha uwezo wa kujilinda wa Ukraine na utatoa nafasi kwa urusi kufanya mashambulizi zaidi ndani ya Ukraine.

Vyanzo: Reuters/AFPE