Marekani na Cuba zafungua ukurasa mpya
18 Desemba 2014Kwanza lilianza tangazo la Rais Barack Obama wa Marekani, ambaye wakati akilihutubia taifa usiku wa jana, alisema wakati wa kubadili muelekeo wa nchi yake kuelekea Cuba umefika. "Leo Marekani inabadilisha mahusiano yake na watu wa Cuba na mageuzi makubwa kabisa kwenye sera yetu ndani ya kipindi cha zaidi ya miaka 50. Tutaumaliza mtazamo wa zamani ambao kwa miongo kadhaa umeshindwa kuendeleza maslahi yetu, na badala yake tutayaweka sawa mahusiano kati ya nchi zetu mbili," alisema Obama kwenye hotuba hiyo.
Muda mchache baadaye, kauli ya Obama ikathibitishwa na Rais Raul Castro wa Cuba, ambaye akilihutubia taifa alisema nchi yake inatambua na inampa heshima anayostahiki Rais Obama kwa hatua zake za kunyoosha mkono wa maridhiano, akaongeza kwamba kutokana na mazungumzo kwa ngazi za juu, yakiwemo yale aliyofanya jana na Rais Obama kwa njia ya simu, "tumeweza kusonga mbele na kutatua maeneo kadhaa yanayohusu maslahi ya mataifa yote mawili."
Kuachiwa kwa majasusi
Katika kile kinachoonekana kutilia nguvu mahusiano haya mapya, Cuba ilimwachia huru raia wa Marekani, Alan Gross, ambaye amekuwa akishikiliwa tangu mwaka 2009, kwa tuhuma za kuingiza nchini Cuba vifaa vya mawasiliano kwa ajili ya ujasusi.
Vile vile, Obama na Castro, walitangaza kwamba nchi zao zilibadilishana majasusi wa kila upande ambao walikuwa wamefungwa upande mwengine.
Hatua hii ya aina yake sasa inaashiria kwamba vikwazo vya kiuchumi na kibiashara kati ya majirani hao ambao wameishi kwa uhasama kwa zaidi ya nusu karne vitaondoshwa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameisifu hatua hii akisema ni ishara njema kwa mataifa yote mawili.
"Habari hii ni njema - kuyaweka sawa mahusiano ya nchi mbili. Kwa hali hiyo, naipongeza sana hatua hii. Ninatarajia kuwa tangazo hili litasaidia kuongeza mualaka baina ya watu wa mataifa hayo mawili ambao wametenganishwa kwa muda mrefu", alisema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.
Marekani kufungua ubalozi Cuba
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, amesema ndani ya kipindi kifupi kijacho, Rais Obama atatuma ujumbe wake maalum nchini Cuba, ambao huenda ukafuatiwa na yeye kuwa waziri wa kwanza wa mambo ya nje wa Marekani ndani ya kipindi cha miaka 60 kuzuru Havana.
Mabadiliko haya ya sera ya Marekani kuelekea Cuba ni matokeo ya mazungumzo ya siri ya miezi 18 yaliyojumuisha mikutano kadhaa nchini Canada na uingiliaji binafsi wa Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis.
Pia yanaakisi hatua isiyo ya kawaida ya Obama bila ya idhini ya bunge katika wakati huu anapomalizia muhula wake wa urais. Obama anapanga kupitia upya sheria ya Marekani inayoitambua Cuba kama taifa linalofadhili ugaidi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Oummilkher Hamidou