1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Cuba zarejesha mahusiano

Admin.WagnerD21 Julai 2015

Marekani na Cuba wamerejesha mahusiano ya kidiplomasia baina yao, baada ya miongo mitano ya uhasama. Uhasama ambao ulianza mnamo mwaka 1961. Hata hivyo leo kila mmoja, atafungua ubalozi katika nchi ya mwenzake.

https://p.dw.com/p/1G1VC
Symbolbild Kuba USA Flaggen
Bendera ya Cuba (kushoto) na bendera ya Marekani (kulia)Picha: picture alliance/Photoshot

Nchi hizo mbili leo (20.07.2015) zinaadhimisha kurejeshwa tena mahusiano ya ngazi ya kidiplomasia yaliyokufa kwa zaidi ya nusu karne, na badala yake ukatanda uhasama. Hii ni hatua muhimu sana kwa nchi hizo mbili, wakiwa wanafunga ukurasa wa uhasama huo wa tangu wakati wa vita baridi.

Enzi mya imeanza, baada ya nchi hizo kukubaliana kurejesha mahusiano ya kawaida kuanzia leo Julai 20. Pale tu ilipogonga saa sita ya usiku jana Jumapili kuingia tarehe ya leo, mahusiano ya nchi hizo mbili yalibadilika.

Uadui huo ulianza wakati wa urais wa John. F. Kennedy pale alipozozana na rais wa wakati huo wa Cuba na mwanamapinduzi Fidel Casto, alipotaka kupanua siasa zake za kisovieti hadi Marekani. Na sasa rais Barack Obama, anarejesha uhusiano na kaka yake Fidel ambaye ni Raul Castro.

Wakati wa majira ya alfajiri wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilipeperusha bendera ya Cuba katika ofisi yake, ikiwa ni miongoni mwa bendera nyengine nyingi za nchi ambazo zina mahusiano ya kidiplomsia na Marekani.

Kuba Präsident Raul Castro im Parlament
Rais wa Cuba Raul CastroPicha: Imago/Xinhua

Mawaziri wa mambo ya nje kukutana rasmi

Mabadiliko hayo ya kihistoria yataadhimishwa baadaye leo, pale maafisa wa Cuba watakapofungua rasmi ubalozi mjini Washington. Na kwa mara ya kwanza bendera ya Marekani itapeperuka ndani ya ofisi ya Cuba, tangu mahusiano yalipovunjika baina yao mwaka 1961.

Nae waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry atakutana na mwenzake wa Cuba, Bruno Rogrigues na kuzungumza na waandishi habari katika mkutano wa pamoja na kutoa taarifa ya pamoja.

Kurejeshwa kwa mahusiano hayo kulitangazwa Disemba 17 mwaka uliopita baada ya rais wa Marekani kukutana na mwenzake wa Cuba Raul Castro, na kukubaliana kuondoa uhasama na kuwa na mahusiano mema. Kilichofuata ni msusururu wa majadiliano yaliyochukua miezi saba, nchi hizo mbili hatimaye zilifanikiwa kuafikiana.

Hata hivyo pande zote mbili zimeonya kuwa mahusiano haya mapya hayatakuwa jambo rahisi, ikizingatiwa uhasama wao uliodumu kwa miongo mitano. Msemaji mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, John Kirby, amesema "bado tuna tofauti zetu ju ya masuala kadhaaa". Hatua hii ya Marekani kurejesha mahusiano na Cuba ni ushindi mkubwa kwa upande wa rais Obama, katika jitihada zake sera za kigeni.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/ape

Mhariri:Josephat Charo