1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Marekani na Japan kuimarisha ushirika kuikabili China

29 Julai 2024

Mawaziri wa ulinzi na wale wa mambo ya nchi za nje wa Marekani na Japan wamekubaliana kutanua ushirikiano wao wa kijeshi na kuiimarisha kamandi ya jeshi la Marekani nchini Japan.

https://p.dw.com/p/4iqI0
Antony Blinken na Yoko Kamikawa
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken na mwenzake wa Japan Yoko Kamikawa.Picha: AP

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mkutano wa waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken na mwenzake wa ulinzi Lloyd Austin pamoja na wenzao wa Japan uliofanyika mjini Tokyo siku ya Jumapili.

Katika hotuba yake ya ufunguzi Waziri Lloyd Austin ameituhumu China kuendekeza tabia za mabavu na kujaribu kubadili uzani wa nguvu na ushawishi kwenye kanda ya Asia Kusini pamoja na eneo zima la Pasifiki.

Viongozi hao wamesema wanachukua hatua hizo za kuimarisha ushirika wao wa kijeshi kutokana na kutanuka na kuimarika kwa uwezo wa China mwenendo unaozingatiwa na nchi hizo mbili kuwa changamoto kubwa ya kiusalama.