Marekani na Korea Kusini zapanga kusitisha Luteka za kijeshi
3 Machi 2019Hatua hiyo ni juhudi za kufufua mazungumzo ya kidiplomasia yatakayowezesha Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa silaha za Nyuklia.
Waziri wa ulinzi wa Korea Kusini Jeong Kyeong Doo na kaimu waziri wa ulinzi wa Marekani Patrick Shanahan wamekubaliana kuwa nchi hizo mbili zitafanya mazoezi madogo ya kijeshi baadaye mwezi Machi.
Wizara ya ulinzi ya Marekani imesema uamuzi huo unatoa ishara ya juhudi za pamoja kati ya Marekani na Korea Kusini za kupunguza wasiwasi uliopo na badala yake kuunga mkono juhudi za kidiplomasia zitakazowezesha kuondoa silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea.
Rais wa Marekani Donald Trump amewahi kuzikosoa luteka hizo za kijeshi akisema kuwa ni ghali na za uchokozi kwa Korea Kaskazini. Korea Kaskazini imekuwa ikiyazingatia mazoezi hayo ya kivita kama njama ya Marekani na Korea Kusini kuivamia nchi hiyo kijeshi.