Marekani na Taliban waandika upya mswada wa kuondoa majeshi
4 Julai 2019Makubaliano hayo pia ni pamoja na kupata uhakikisho madhubuti wa Taliban wa kupambana na ugaidi kabla ya mkutano wa amani kwa ajili ya makundi yote ya Afghanistan utakaofanyika siku ya Jumapili.
Maafisa ambao wako karibu na majadiliano hayo, lakini ambao hawana mamlaka ya kuyazungumzia , wanasema majadiliano yameingia katika nyakati za usiku jana Jumatano na wajumbe watarejea tena leo Alhamis katika mazungumzo, hayo ya ana kwa ana ambayo yamechukua siku sita kati ya wapiganaji hao na mjumbe wa Marekani Zalmay Khalilzad.
Suhail Shaheen, msemaji wa ofisi ya kisiasa ya Taliban nchini Qatar , mapema aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba mswada wa makubaliano unaandikwa upya kujumuisha vipengee vilivyokubaliwa kwa pamoja. Pande hizo mbili bado zimegawika kuhusiana na muda wa kuyaondoa majeshi, wakati Marekani inataka muda zaidi.
Maafisa wa Taliban , ambao walizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina, wamesema Marekani inataka miezi 18 kukamilisha kuviondoa vikosi vyake vyote hata kama rais wa Marekani Donald Trump amekiambia kituo cha televisheni cha Fox News mapema wiki hii kuwa uondoaji wa vikosi tayari umeanza kimya kimya na kwamba nguvu za vikosi hivyo imepunguzwa hadi wanajeshi 9,000. Taarifa ya rais Trump imekuwa tangu wakati huo ikikinzana na taarifa za maafisa waandamizi wa Marekani, ambao wamesema nguvu ya majeshi hayo haijabadilika na iko katika jumla ya wanajeshi 14,000.
Dhamira ya Trump
Pamoja na hayo, taarifa ya Trump imeimarisha dhamira ya rais huyo ambayo mara kwa mara amekuwa akieleza ya kujitoa kutoka Afghanistan na kufikisha mwisho vita hivyo vya Marekani vilivyodumu kwa muda wa miaka 18, vita virefu kabisa katika historia.
Nia yake hiyo ya kuondoa majeshi imeimarisha nafasi ya Taliban , kundi ambalo linadhibiti nusu ya nchi na kupata maridhiano muhimu katika kupanga mkutano unaokuja wa amani , ambao hautajumuisha ujumbe wowote rasmi kutoka katika serikali ya Afghanistan.
Ujerumani na Qatar , nchi ambazo zinasimamia kwa pamoja majadiliano na kutoa mialiko, zimesema washiriki "watahudhuria tu , kama wajumbe binafsi, " shari ambalo rais Ashraf Ghani amelipinga kwa nguvu kabisa. Hajazungumzia lolote kuhusu mkutano wa Jumapili.
Taliban wamekataa kabisa kuzungumza na serikali ya Ghani, wakiita kibaraka wa Marekani, lakini wamesema maafisa wa serikali wanaweza kuhudhuria mkutano huo kama raia wa kawaida.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Mohamed Khelef