1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO kufanya kikao kujadili masuala ya kiusalama ya Uturuki

28 Julai 2015

Marekani na Uturuki zimekubali kushirikiana kupambana dhidi ya wanamgambo wa IS kaskazini mwa Syria huku Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu akiapa kuendelea na mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa kikurdi PKK

https://p.dw.com/p/1G5bS
Picha: John Thys/AFP/Getty Images

Uturuki ambayo kwa muda sasa imekuwa ikisita kujiunga na kampeini ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi linalojiita dola la kiislamu IS hatimaye imekubali kushirikiana na Marekani katika mapambano hayo.

Msimamo huo wa Uturuki unakuja huku mabalozi wa nchi zote 28 wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO wakikutana hii leo katika makao makuu ya jumuiya hiyo mjini Brussels, Ubelgiji kufuatia ombi la Uturuki kutaka kuijadili kampeini yake dhidi ya IS na wanamgambo wa kikurdi.

Uturuki imezidi kuwaghadhabisha wakurdi ambao ni jamii ya walio wachache nchini humo kwa kufanya mashambulizi katika kijiji kinachodhibitiwa na wakurdi kaskazini mwa Syria huku ndege zake za kijeshi zikiendelea kuzishambulia ngome za wanamgambo wa kikurdi kaskazini mwa Iraq.

Waasi wa Syria kusaidiwa na Uturuki na Marekani

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa marekani ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Uturuki na Marekani zinalenga kuunda eneo salama lililo huru dhidi ya mashambulizi na udhibiti wa IS na kuhakikisha usalama na uthabiti unaimarishwa katika eneo la mpaka kati ya Uturuki na Syria.

Türkei Luftangriffe auf Kurden im Irak
Ndege ya kivita ya Uturuki aina ya F 16 iliyoshambulia ngome za PKK IraqPicha: Reuters/M. Sezer

Nchi hizo mbili zimetangaza kuwepo mipango ya kutoa ulinzi wa angani kwa waasi wa Syria wenye msimamo wa wastani na kuhakikisha pia kuna maeneo salama kwa maelfu ya raia wa Syria wanaoyatoroka mapigano kaskazini mwa nchi hiyo. Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema waasi wa Syria wanaolengwa ni wenye msimamo wa wastani.

Uturuki hivi sasa inawahifadhi takriban wasyria milioni moja na laki nane. Hata hivyo kumeibuka maswali iwapo Uturuki inadhamiria kupambana na IS au nia yake kuu ni kukabiliana na wanamgambo wa kikurdi nchini Syria na Iraq.

Davutoglu amesema Uturuki itasonga mbele na operesheni zake za kijeshi dhidi ya wanamgambo wa kundi lililoharamishwa la Kurdistan Workers' Party PKK hadi kundi hilo lipokonywe silaha kuamabatana na makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2013 ya kundi hilo kuweka chini silaha.

PKK imekuwa ikifanya uasi kwa miongo mingi kusini mashariki mwa Uturuki lakini ina ngome chache kaskazini mwa Iraq. Uturuki imekuwa ikilichukulia kundi la wapiganaji wa kikurdi linalopambana na IS Syria la Democartic Union Party PYD kama tawi la PKK nchini Syria.

Uturuki ina haki ya kujilinda dhidi ya PKK

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani John Kirby amesema Uturuki ina haki ya kujilinda dhidi ya PKK kundi ambalo Marekani pia imeliorodhesha kama la kigaidi msimamo unaoungwa mkono pia na katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg
Katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens StoltenbergPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Hata hivyo Uturuki imeonywa na Stoltenberg na Rais wa Ufaransa Francois Hollande kuwa muangalifu katika mashambulizi yake dhidi ya wakurdi kwa kutolilenga kundi lisilokusudiwa kati ya makundi hayo mawili ya wapiganaji na kutatiza juhudi za miaka mingi za kutafuta suluhisho la amani kati ya serikali ya Uturuki na wapiganaji wa kikurdi.

Wapiganaji wa kikurdi wanaoungwa mkono na Marekani katika kupambana dhidi ya IS kaskazini mwa Syria jana waliukomboa mji muhimu wa Sarrine ulioko mashariki mwa mji wa Kobane lakini wameishutumu Uturuki kwa kuwashambulia. Kiasi ya wapiganaji wanne na raia kadhaa walijeruhiwa katika mashambulizi ya angani yaliyofanywa na Uturuki ambayo imekanusha iliwalenga kimakusudi wapiganaji hao wa YPG.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga