1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Uchaguzi Libya ni suala la msingi

23 Juni 2021

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken amesema ni suala la msingi kwa Libya kufanya uchaguzi ifikapo mwezi Disemba ili kurejesha amani kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi.

https://p.dw.com/p/3vRUe
Deutschland Berlin | US-Außenminister Blinken | Treffen mit Maas
Picha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

Blinken pia amezitolea mwito pande zinazojihusisha na mzozo uliodumu kwa muda mrefu nchini humo kuwaondoa wapiganaji wa kigeni ili kufungua njia ya kufanyika uchaguzi huo. 

Blinken amesema mjini Berlin kwamba ipo fursa ambayo haiwajawahi kujitokeza katika miaka ya karibuni ya kuisaidia Libya kusonga mbele ikiwa salama na huru.

Ujerumani na Umoja wa Mataifa wameandaa mkutano huo wa siku moja unaolenga kuimarisha juhudi za kurejesha amani katika taifa la Libya, linalokabiliwa na mzozo, unaoihusisha pia serikali ya kitaifa ya mpito ya Libya na mataifa yenye ushawishi  yanayohusika kwenye mzozo huo kwa lengo la kuimarisha hatua ya usitishwaji mapigano na kusaidia Libya katika mchakato wa kisiasa na kumaliza uingiliaji wa nje.

Soma Zaidi: Muda wa kuondoka vikosi vya kigeni nchini Libya wamalizika 

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas, amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya kumkaribisha Blinken mjini Berlin kwamba wanataka Libya kurejea kwenye amani na utulivu, kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa.

"Libya ni mfano mzuri katika jukwaa la kimataifa wa kwamba tunaweza kutatua mizozo kwa njia za kisiasa. Na kulipigwa hatua nzuri nchini humo katika miezi michache iliyopita, usitishwaji mapigano unaendelea na leo tunataka kuhakikisha kwamba hali inaendelea kuwa hivyo. " alisema Maas  

Libyen Dbeibah wiedereröffnet die Straße Misrata - Sirte
Waziri mkuu wa mpito nchini Libya Abdulhamid Dbeibah akiwapungia raia baada ya barabara inayounganisha eneo la mashariki na magharibi nchini humo kufunguliwa baada ya miaka miwili.Picha: Mahmud Turkia/Getty Images/AFP

Ameahidi pia kwamba watalisaidia taifa hilo kimaendeleo na kiuchumi, kwa kuwa uwezo huo wanao, huku akisisitiza ni lazima taifa hilo lifanye uchaguzi kama ilivyopangwa.

Aidha, Maas ameendelea kuyatolea mwito mataifa ya nje yaliyoahidi kuwaondoa wanajeshi wao katika mkutano wa kwanza kama huo uliofanyika mjini Berlin mapema mwaka jana kutimiza ahadi zao, ili kuiruhusu Libya kuamua kuhusu mustakabali wa taifa lao.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba bado kuna wapiganaji wa kigeni na mawakala 20,000 nchini Libya. Na uwepo huo unachukuliwa kama kitisho kwa serikali ya mpito inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, kuelekea kwenye uchaguzi huo wa Disemba 24.

Mwanadiplomasia mmoja, aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa amesisitizia kuhusu hali tete nchini humo, akisema suluhu haiwezi kupatikana kwa muda mfupi. Lakini pia ameelezea matumaini yake kwamba huenda kukapigwa hatua kwenye mkutano wa hii leo kwa kuwa hakuna taifa litakalonufaika na mzozo huo iwapo utaibuka upya.

Mtaalamu wa masuala yahusuyo Libya Jalel Harchaoui wa taasisi ya Global Initiative naye anaamini mazungumzo haya yanaweza kuwa na msaada mkubwa katika uchaguzi huo unaokuja.

Soma Zaidi: Ujerumani yaandaa kongamano kuhusu Libya 

Mashirika: DPAE/RTRE