1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yailaumu Urusi kuanguka ndege ya Malaysia

19 Julai 2014

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power amekiambia kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Marekani haiondoi uwezekano kuwa Urusi ilihusika.

https://p.dw.com/p/1CfPC
UN-Sicherheitsrat 2011
Baraza la Usalama likifanya kikao cha dharuraPicha: AP

Balozi Samantha Power amesema Urusi ilisaidia katika kurushwa kwa kombora la kutokea ardhini kwenda angani ambalo liliiangusha ndege ya shirika la ndege la malaysia katika anga ya Ukraine, na kusababisha watu 298 waliokuwa katika ndege hiyo kuuwawa.

Power amesema kuwa Marekani inaamini huenda ndege hiyo iliangushwa na kombora la SA-11 lililofyatuliwa kutoka katika eneo la mashariki mwa Ukraine linalodhibitiwa na watu wanaotaka kujitenga wanaounga mkono Urusu. Amesema Urusi imetoa kombora hilo la SA-11 pamoja na silaha nyingine kwa watu hao wanaotaka kujitenga.

UN Debatte zur Ukraine 13.04.2014 Samantha Power
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha PowerPicha: Don Emmert/AFP/Getty Images

Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Mark Lyall Grant, ambaye ameitisha kikao hicho cha dharura, alikuwa mkali zaidi katika kuelekeza lawama zake kuhusu mkasa huo wa kuangushwa kwa ndege hiyo ya abiria.

Waasi wanahusika

"Ni wazi kabisa nani anahusika: kutokana na ghasia zisizo na maana za watu wanaotaka kujitenga na wale ambao wanaunga mkono, kutoa vifaa na ushauri kwao," amesema balozi huyo. "Baraza linapaswa kuwa pamoja katika kushutumu vitendo hivi, na kudai kuwa makundi haya yanyang'anywe silaha , yajizuwie na matumizi ya silaha pamoja na uchokozi na kuanza kujishughulisha na majadiliano kupitia njia za kidemokrasia ambazo zipo kwao.

Ndege hiyo ya abiria ya shirika la ndege la Malaysia ilikuwa ikisafiri katika umbali wa mita 10,000 kutoka usawa wa bahari ikitokea Amsterdam nchini Uholanzi kwenda Kuala Lumpur katika eneo linalojulikana la safari za ndege wakati ilipotunguliwa kwa kombora siku ya Alhamis, Power amesema.

Karte Route des Fluges MH17 bis zum Absturz Englisch
Njia ya safari za anga kupitia Ukraine

Power amesema kuwa mapema Alhamis mwandishi habari aliripoti kuona kifaa cha mfumo wa kurushia kombora la SA-11 katika eneo linalodhibitiwa na wanaotaka kujitenga karibu na mji wa Snizhne, "na wanaotaka kujitenga walionekana saa chache kabla ya tukio hilo wakiwa na gari lililobeba mfumo wa kurushia makombora ya SA-11 karibu na eneo ambalo ndege hiyo iliangushwa.

Power hakuweza kumtambua mwandishi huyo. Lakini siku ya Alhamis , mwandishi habari wa shirika la habari la AP ameona mashine ya kurushia maroketi karibu na Snizhne.

Wachunguzi wa kimataifa

Wachunguzi wa kimataifa walitarajiwa kuanza juhudi nyingine leo Jumamosi(19.07.2014)kuingia katika eneo lililoangukia ndege hiyo ya shirika la ndege la Malaysia mashariki mwa Ukraine, baada ya kuzuiwa na watu wenye silaha wanaotaka kujitenga wanaounga mkono Urusi.

Niederlande Air Malaysia Trauer
Maombolezo nchini UholanziPicha: Christopher Furlong/Getty Images

Wachunguzi kutoka shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE, ambao si wataalamu wa masuala ya utambuzi katika eneo la tukio, wamefika katika eneo hilo karibu na mpaka wa Ukraine na Urusi lakini walikataliwa kuingia katika eneo hilo la mabaki ya ndege na waasi ambao wanadhibiti eneo hilo, amesema mwenyekiti Thomas Greminger.

Wafanyakazi wa huduma za dharura katika matukio wa Ukraine wamewasili katika eneo hilo lakini waasi wanajaribu kuvuruga juhudi zao za uokozi, amesema Serhiy Taruta, gavana aliyeteuliwa na serikali mjini Kiev katika jimbo la Donetsk.

Obama amshutumu Putin

Katika ikulu ya Marekani rais Barack Obama ameitolea mwito Urusi , wale wanaotaka kujitenga na wanaounga mkono Urusi pamoja na Ukraine kusitisha mapigano mara moja ili kuruhusu uchunguzi ufanyike.

Obama hakusema iwapo Marekani inaamini kuwa ndege hiyo ya abiria ilishambuliwa kwa makusudi ama n ilishambuliwa kwa kudhania kuwa ilikuwa ndege ya uchukuzi ya jeshi la Ukraine, Amejizuwia kutoa lawama kwa waasi.

US Präsident Barack Obama Rede
Rais barack ObamaPicha: picture-alliance/dpa

Rais wa Urusi Vladimir Putin anabeba lawama za kuendeleza mzozo huo wa mashariki ya Ukraine, ambao Urusi imesaidia kuuanzisha kwa kuliunganisha eneo la rasi la Crimea mwezi Machi, Obama amesema.

Rais wa China Xi Jinping ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haki na wenye malengo kuhusiana na kuangushwa kwa ndege hiyo ya shirika la ndege la Malaysia Boeing 777 ikiwa na watu 298. Uchunguzi huo unapaswa kutafuta ukweli haraka iwezekanavyo, tovuti ya rais Xi imesema.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae / ape

Mhariri: Sudi Mnette