Marekani yaionya Iran dhidi ya kuwashambulia raia wake
13 Januari 2020Haya yamejiri wakati ambapo waziri wa ulinzi wa Marekani Mark Esper amesema milango iko wazi kwa Iran kufanya mazungumzo na Marekani bila masharti yoyote.
Ujumbe huu wa Trump umekuja wakati ambapo uongozi wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu unakabiliwa na changamoto kutoka kwa waandamanaji walio na hasira baada ya nchi yao nusra iingie kwenye vita na Marekani baada ya mashambulizi ya kulipiziana kisasi.
Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Trump ameeleza kuwa ulimwengu na hasa Marekani inatazama yanayoendelea nchini humo kwa sasa. Lakini licha ya onyo la rais huyo wa Marekani, vidio zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha polisi ya Iran na majeshi yakifyatua risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji karibu na eneo la Azadi ambapo baadhi ya waandamanaji wameonekana wakivujwa na damu.
Canada haitopumzika hadi haki ipatikane
Lakini mkuu wa polisi mjini Tehran Hossein Rahimi amekanusha hayo akisema maafisa wake wamepewa masharti ya kutowakabili waandamanaji.
Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu nayo yamejitokeza na kuitaka Jamhuri hiyo ya Kiislamu kuwaacha raia kuandamana kwa amani kama inavyoruhusu katiba ya nchi hiyo.
Kufariki kwa watu wote 176 waliokuwa kwenye ndege iliyodunguliwa wiki iliyopita na kukiri kwa Iran baadae kwamba kikosi chake kiliilenga ndege hiyo kimakosa kwa kufikiri kuwa lilikuwa ni kombora ndilo jambo lililosababisha maandamano kote nchini humo.
Canada ambayo ilikuwa na idadi kubwa ya wahanga katika tukio hilo inaendelea kuomboleza huku Waziri mkuu Justin Trudeau akiahidi haki kwa familia zilizowapoteza wapendwa wao.
"Nataka kuzihakikishia familia zote na Wacanada wote, hatutapumzika hadi tutakapopata majibu, hatutopumzika hadi kutakapokuwa na haki na uwajibikaji," alisema Waziri Mkuu Justin Trudeau.
Iran ilitangaza haitotii tena mkataba wa nyuklia
Huku hayo yakijiri Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wametoa wito kwa Iran kuendelea kutekeleza mkataba wa mwaka 2015 ambao unadhibiti mpango wa nyuklia wa nchi hiyo. Kansela Angela Merkel, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson wameyasema haya katika taarifa ya pamoja waliyoitoa Jumapili jioni.
Mkataba huo ulitiwa saini kati ya Iran na wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao ni Marekani, Urusi, China, Ufaransa na Uingereza pamoja na Ujerumani na Umoja wa Ulaya.
Wiki iliyopita Iran ilitangaza kwamba haitoendelea kuuheshimu mkataba huo kufuatia kuuwawa kwa kamanda wake wa ngazi ya juu Qasseim Soleimani na Marekani.