Marekani yaishutumu Urusi kwa kufadhili vita Sudan
7 Januari 2025Akizungumza katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumatatu, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield, ameishutumu Urusi kwa kusema ilichagua kuweka kizuizi, kusimama peke yake na kuweka raia hatarini:
"Baraza hili lilikutana miezi miwili tu iliyopita kujadili azimio la kutaka kusitishwa kwa mapigano nchini kote, kuongeza ulinzi wa raia na mtiririko wa misaada usiozuiliwa."
"Wanachama 14 wa baraza waliidhinisha maandishi yaliyotayarishwa na Sierra Leone na Uingereza na bado, Urusi, ilichagua kuweka kizuizi, ikisimama peke yake ilipopiga kura kuwahatarisha raia huku ikifadhili pande zote mbili za mzozo."
Alipoulizwa kuhusu maelezo zaidi katika madai yake, Balozi Greenfield, alisema Washington inafahamu kuhusu maslahi ya Urusi katika biashara ya dhahabu ya Sudan na inalaani msaada wa aina yeyote kwa pande zinazopigana ima kupitia biashara haramu ya dhahabu au kupeana zana za kijeshi.
Soma pia: Raia kumi wauawa kwenye mashambulio ya anga Sudan
Aidha Greenfield ameeleza kwamba wanaamini ushirikiano wa mamlaka ya Sudan katika uchimbaji dhahabu na makampuni yaliyowekewa vikwazo ya Urusi pamoja na watu binafsi wanaweza kuzidisha kwa muda mrefu matarajio ya Wasudan ya kukomesha vita.
Urusi yaikosoa Marekani
Kujibu, madai ya Marekani naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Dmitry Polyanskiy alisema nchi yake inasikitika kwamba Marekani inajaribu kuhukumu mataifa mengine yenye nguvu duniani kwa kipimo chake.
Aidha Polyanskiy ameikosoa Marekani akisema inajaribu kuhifadhi kwa namna yoyote, uhusiano wake na mataifa mengine kwa misingi ya uporaji na miradi ya uhalifu inayolenga kuitajirisha Marekani.
Mgogoro wa kibinaadamu usio kiafani
Huku haya yakijiri Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kupatikana kwa dola za kimarekani bilioni 4.2 kwa lengo la kuwasaidia watu milioni 20.9 kote nchini Sudan.
Soma pia: Umoja wa Mataifa wasema zaidi ya wasudan milioni 30 wanahitaji msaada.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Uendeshaji na Utetezi, wa OCHA, Edem Wosornu, amesema utafiti wa Uainishaji wa Awamu ya Usalama wa Chakula Jumuishi (IPC), unaonyesha hali ya njaa katika maeneo matano, ikiwa ni pamoja na kambi za Zamzam, Al Salam, na Abu Shouk, pamoja na Milima ya Nuba ya magharibi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu milioni 30.4 wanahitaji msaada katika nchi hiyo inayokabiliwa na mgogoro wa kibinadamu usio kifani.