Marekani yaitisha mkutano wa UN dhidi ya Korea Kaskazini
15 Septemba 2018Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha mkutano wa dharura kujadili kile kinachotajwa na Marekani kama juhudi za baadhi ya nchi za kupinga vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini.
Katika taarifa, ujumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa umesema ajenda ya mazungumzo hayo itakuwa ni kujadili utekelezaji wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini vyenye lengo la kuishinikiza nchi hiyo kuachana na shughuli zake za kutengeneza silaha za nyuklia.
Marekani imeishutumu Urusi kwa kubadilisha ripoti ya kujitegemea ya Umoja wa Mataifa, na kuficha maelezo yanayosema kampuni za Urusi zimekiuka vikwazo hivyo vilivyowekwa dhidi ya Korea Kaskazini.
China na Urusi ni kati ya wakiukaji wakuu
Awali Marekani ilizishutumu Urusi na China kwa kusafirisha mafuta ya petroli kwenda Korea Kaskazini kinyume na sheria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo Ijumaa ameishutumu Urusi kwa kuchukua hatua za kuhujumu vikwazo hivyo vya kimataifa, ambavyo viliafikiwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2006 na baadae kuimarishwa zaidi kwa lengo la kuudhoofisha uchumi wa Korea Kaskazini.
"Urusi imekuwa ikijaribu kuhujumu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kazi ya kamati ya Umoja wa Mataifa inayotathmini utekelezaji wa vikwazo," amesema katika mkutano wake mfupi na waandishi habari katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Pompeo amesema anatumai kamati ya Umoja wa Mataifa inayosimamia utekelezaji wa vikwazo "itachapisha nyaraka ya awali... inayoonyesha wazi vitendo vinavyahusiana na ukiukaji wa vikwazo vya kimataifa."
Biashara ya magendo ya makaa ya mawe na silaha
Ripoti hiyo, ambayo imewasilishwa mwezi uliopita katika kamati ya kusimamia utekelelezaji wa vikwazo ya Baraza la Usalama, imeonya kwamba Korea Kaskazini haikusimamisha mipango yake ya kutengeneza silaha za nyuklia na makombora. Na pia inakiuka vikwazo ilivyowekewa na Umoja wa Mataifa dhidi ya mauzo ya bidhaa zake nje ya nchi. Ripoti hiyo pia imesema taifa hilo limekuwa likikiuka vikwazo katika usafirishaji shehena za silaha na vikwazo vya kifedha ilivyowekewa.
Mwezi Julai, Marekani imeishutumu Korea Kaskazini kwa usafirishaji wa bidhaa za petroli iliyosafishwa kwa njia za magendo na kupindukia kikomo kinachoruhusiwa kila mwaka chini ya vikwazo ilivyowekewa cha mapipa 500,000.
China, ambayo ni mshirika mkuu wa Korea Kaskazini, inashutumiwa kuhusika na asilimia 90 ya biashara ya taifa hilo lilotengwa na dunia.
'Vitendo vya kihalifu'
Uhalifu mwengine uliotajwa na Marekani ni pamoja na wizi wa mitandaoni pamoja na vitendo vengine vya kihalifu, ambavyo Pompeo awali alisema "vinaipatia fedha nyingi serikali ya Korea Kaskazini na lazima vizuiwe."
Ijumaa, amesema Marekani itafanya mazungumzo na Korea Kaskazini juu ya jinsi ya "kutekeleza ahadi zote zilizotolewa" Juni 12 katikia mkutano wa kilele kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.
Mapema mwaka huu, Marekani ilidai kwamba vikwazo ilivyowekewa Korea Kaskazini vimezuia usafirishaji bidhaa nje ya nchi, ambao unajumuisha asilimia 90 ya biashara yake.
Wanadiplomasia wengi wanavisifu vikwazo hivyo kwa kuweza kupunguza uhasama katika uhusiano wa kati ya Marekani na Korea Kaskazini, pamoja na kuwezesha kufanyika mkutano wa mwezi Juni kati ya Trump na Kim, ambapo wamekubaliana kuondoa kabisa silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/dw, AP, dpa, Reuters
Mhariri: Isaac Gamba