1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaiwekea vikwazo Ethiopia na Eritrea

24 Mei 2021

Marekani imeweka vikwazo vya kusafiri kwa maafisa wa Ethiopia na Eritrea wanaotuhumiwa kuchochea vita katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia, ikisema waliohusika hawajachukua hatua zozote za maana kuumaliza mzozo huo.

https://p.dw.com/p/3tqkk
Äthiopien I Konfliktregion Tigray
Picha: Ethiopian News Agency/AP/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema vikwazo hivyo vitamuhusu afisa yeyote wa sasa na wa zamani wa serikali za Ethiopia au Eritrea, maafisa wa vikosi vya usalama au watu binafsi waliohusika kudhoofisha azimio la kupatikana kwa amani ya Tigray, wakiwemo wapiganaji wa Amhara na maafisa wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF.

Msaada wa kiutu wazuiwa

Blinken amesema watu katika jimbo la Tigray wanaendelea kuumia kutokana na ukiukaji wa haki za binaadamu, mateso, na ukatili mwengine, na msaada wa kiutu unaohitajika kwa dharura unazuiwa na wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea.

Mwanadiplomasia huyo wa Marekani amesema licha ya kuwepo juhudi kubwa za kidiplomasia, pande zote zinazohusika katika mzozo wa Tigray hazijachukua hatua zozote za maana kumaliza uhasama au kulifuata azimio la amani la mzozo wa kisiasa.

US-Außenminister Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony BlinkenPicha: Saul Loeb/Pool AFP/AP/picture alliance

''Marekani inalaani vikali mauaji, watu kuondolewa kwa lazima kwenye makaazi yao, unyanyasaji wa kingono na ukiukaji mwingine wa haki za binaadamu na ametoa wito wa kupatikana kwa suluhisho la kisiasa na la kudumu kuhusu mzozo huo na jumuia ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua sasa,'' alifafanua Blinken.

Blinken pia ametangaza kuweka vikwazo vinavyohusu msaada wa kiuchumi na usalama kwa Ethiopia, akiongeza kuwa Marekani itaendelea kutoa msaada wa kiutu katika maeneo kama vile ya afya, chakula na elimu.

Maelfu ya watu wameuawa na wengine wamelazimika kuyakimbia makaazi yao kwenye jimbo la Tigray tangu mwezi Novemba, mwaka uliopita baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed kupeleka majeshi yake kupambana na viongozi wa chama cha TPLF katika jimbo hilo.

Bildergalerie Äthiopien | Flucht aus der Region Tigray
Baadhi ya wakaazi wa Tigray wakisubiri msaada wa chakulaPicha: Baz Ratner/REUTERS

Majeshi ya Eritrea ambayo yaliungana na jeshi la Ethiopia yameshutumiwa kwa kufanya ukatili dhidi ya raia walioko kwenye eneo la mpaka. Jumuia ya kimataifa imetoa wito wa kurejeshwa amani, huku Umoja wa Mataifa na Marekani zikiendelea kushinikiza kuondolewa kwa majeshi kwenye jimbo hilo.

Ethiopia na Eritrea zatangaza kuondoa majeshi yake

Mataifa yote mawili yametangaza kuyaondoa majeshi yake, ingawa hata hivyo bado hayajatekeleza hatua hiyo. Kwa mara ya kwanza siku ya Ijumaa Ethiopia iliyatuhumu majeshi ya Eritrea kwa kuwaua raia 110 katika mauaji mwezi Novemba katika jimbo la Tigray.

Katika taarifa za awali, mashirika makubwa ya kimataifa ya kutetea haki za binaadamu ya Human Rights Watch na Amnesty International, yaliyashutumu majeshi ya Eritrea kupigana Tigray na yalisema kwamba wengi wa watu waliouawa walikuwa ni raia.

(AP, DPA, AFP)