Marekani yajiunga uchunguzi ajali ya Ndege
12 Machi 2019Hayo yanajiri wakati mashirika zaidi yamesitisha matumizi ya ndege aina ya Boeing chapa 737 Max 8.
Maafisa kutoka Mamlaka inayoshughulikia usafiri wa anga nchini Marekani wamejiunga na timu ya uchunguzi nchini Ethiopia kwa kulitembelea eneo ambalo ajali ilitokea nje kidogo ya mji mkuu wa Ethiopia Addis Abbaba.
Mamlaka hiyo imesema inatumai kuwa kampuni ya ndege ya Boeing itaufanyia marekebisho ya haraka mfumo wa uendeshaji ndege ambao unahisiwa kuwa chanzo cha ajali ya pili ya ndege chapa 737 Max 8.
Kadhalika kampuni ya Boeing itapaswa kutoa muhtasari mpya wa mafunzo na kuchapisha kabrasha nyingine za miongozo ya uendeshaji ndege ya Max 8
Kampuni ya Boeing yenyewe ilitoa taarifa hapo jana ikisema ilikwisha anza kufanya kazi kwa karibu na mamalaka ya usafiri wa anga tangu ajali ya Lion Air ilipotokea mwaka uliopita ili kuunda mfumo ulioboreshwa wa uendeshaji ndege utakaofungwa kwenye ndege zote chapa 737 Max 8.
Max 8 inapitia kipindi kigumu
Ndege chapa Max 8 ambayo ni toleo la karibuni kabisa la kampuni ya Boeing ni miongoni mwa zilizouzwa kwa wingi kabisa duniani lakini hatma yake inaweza kuwa hatarini kutokana na ajali mbili zilizoihusisha ikiwemo ya siku ya jumapili.
Australia na Singapore zimetangaza leo kuzipiga marufuku ndege chapa Max 8 kwenye anga zake zikijiunga na nchi nyingine kadhaa ambazo zimechukua hatua ya aina hiyo tangu mkasa wa mwishoni mwa juma.
Australia imesema hatua hiyo ni ya muda wakati inasubiri taarifa muhimu kuhusu tathmini ya usalama wa ndege hizo.
China, Indonesia, Argentina na kampuni ya ndege ya Ethiopia yenyewe tayari zilikwishatangza kusitisha matumizi ya chapa Max 8.
New Zealand kwa upande wake haijapiga marufuku matumizi ya ndege hizo na kwenye taarifa yake iliyotolewa leo imesema imethibitisha kuwa ndege chapa Max 8 ni salama.
Hisa za Boeing zaporomoka
Wasiwasi kuhusu aina hiyo ya ndege umesababisha kuanguka kwa hisa za kampuni ya Boeing kwa asilimia 13.5 hapo jana ikiwa ni kiwango cha chini kabisa katika kipindi cha miongo miwili.
Siku ya jumatatu wachunguzi walifanikiwa kuvipata visanduku viwili vyeusi vya kutunza kumbukumbu za safari ya ndege ambavyo vitakuwa chanzo cha uhakika kutoa sababu za ajali hiyo.
Ingawa afisa mmoja alikaririkiwa akisema kuwa moja ya kisanduku kimeharibika kwa kiasi fulani lakini wachunguzi wametoa ahadi ya kujaribu kupata taarifa zilizorikodiwa
Mwandishi: Rashid Chilumba/AP7AFP
Mhariri: Sekione Kitojo