Maandamano huko yarindima Cuba
14 Julai 2021Serikali ya Cuba imezima huduma za mitandao ya kijamii na mawasiliano ya ujumbe mfupi,kuanzia Facebook mpaka Whatsapp wakati nchi hiyo ikikabiliwa na maandamano makubwa ya kuipinga serikali,maandamano yaliyozuka tangu siku ya Jumapili.
Maandamano ya Cuba yalizuka ghafla na kuzagaa katika miji chungunzima siku ya Jumapili wakati nchi hiyo ikiwa katika hali ngumu kabisa ya kiuchumi ambayo haijawahi kuonekana kwa miaka 30 iliyopita.
Kuna ukosefu mkubwa wa umeme,chakula na dawa,lakini waziri wa mambo ya nje Bruno Rodriguez anasema hakuna njaa nchini humo.
"Ni kweli kwamba kuna ukosefu wa data za simu za mkononi tangu serikali ilipozima mawasiliano,lakini pia kuna ukosefu wa dawa ,na ni kweli kwamba hakuna njaa nchini Cuba lakini kuna mambo ya msingi ''
Rais wa Marekani mnamo siku ya Jumatatu alisema nchi yake inasimama imara na wananchi wa Cuba wakati wakidai haki zao za msingi huku msemaji wa wizara ya mambo ya nje Ned Price akiitaka serikali ya Cuba kufungua huduma zote za mawasiliano zilizozimwa.
Iran imeikosoa Marekani kwa kuingilia masuala ya ndani ya Cuba kufuatia maandamano hayo ya Cuba,nchi ya kisiwa ya utawala wa kikomunisti na ambayo kwa miongo imekuwa ikikabiliwa na vikwazo vya Marekani.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Saeed Khatibzadeh ametowa taarifa Jana akisema wakati Marekani inawajibika binafsi kwa matatizo mbali mbali ya wananchi wa Cuba,sasa inajitokeza kuunga mkono maandamano nchini humo na huko ni kutafuta kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nje ya Iran nchi ambayo pia iko kwenye adha inayosababishwa na vikwazo vya Marekani,ameweka wazi mshikamano wa nchi yake na watu na serikali ya Cuba.
Cuba yenyewe imeilaumu Marekani kwa kuendelea kufuata sera ya kuikandamiza kiuchumi kwa lengo la kuchochea vurugu za kijamii ndani ya Cuba. Mtu mmoja ameuwawa na wengine zaidi ya 100 akiwemo mwandishi habari wa kujitegemea na wapinzani walikamatwa wakati wa maandamano ambapo baadhi yao bado kufikia jana Jumanne walikuwa wakishikiliwa rumande,kwa mujibu wa taarifa za waangalizi na wanaharakati.
Tangu mwaka 1962 Cuba iko chini ya vikwazo vya Marekani na hadi wakati huu serikali ya mjini Havana inasema Marekani inaonesha dhamira ya wazi wa kuendeleza sera ya kuimaliza kiuchumi.
Na tangu mapinduzi ya kiislamu ya Iran yaliyouangusha utawala wa Shah ulioungwa mkono na Marekani nchi hiyo ya Iran na Cuba zimekuwa katika kawaida ya kusaidiana kidiplomasia. Jamhuri ya kiislamu ikilaani vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba na serikali ya mjini Havana nayo ikiiunga mkono Tehran katika haki yake ya kuwa na nishati ya Nuklia kwa ajili ya matumizi ya kiraia.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Iddi Ssessanga