Marekani yalaani shambulizi kwa raia wake
6 Julai 2014Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Jen Psaki amethibitisha kuwa mtoto huyo Tariq Khdeir, mwenye umri wa miaka 15 anazuiliwa na Israel na kwamba afisa wa ubalozi wa Marekani alimtembelea jana Jumamosi.
"Tuna wasiwasi kuhusu ripoti kuwa alipigwa vibaya alipokuwa anashikiliwa na polisi, na tuna laani aina yoyote ya matumizi ya nguvu ya kupita kiasi.
Tunatoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka na wa uwazi na wa kuaminika juu ya hili. Tunataka waliohusika katika matumizi ya nguvu ya aina yoyote wawajibike. " Alisema Psaki.
Baraza la mahusiano ya wamarekani waislamu, nchini Marekani imeongeza sauti yake kwa kusema kuwa Khdeir ni mzaliwa wa Marekani na kuiomba wizara ya mambo ya nchi za nje kufanya kila juhudi ili kijana huyo aachiwe.
Aidha video ambayo imekuwa ikisambazwa katika mitandao ya kijamii imeonyesha polisi wawili wakimpiga kijana huyo kabla ya kumbeba na kwenda naye. Katika Video nyengine iliotolewa katika mitandao inaonesha uso wa khdeir, jicho na mdomo ikiwa imevimba.
Familia ya Khdeir iliotokea Tampa, Florida Marekani, ilikuwa inawatembelea jamaa zao Mashariki mwa Jerusalem.
Kijana huyo wa miaka 15 ni binamu wa Mohammed Hussein Abu-Khdeir, kijana aliye na umri wa miaka 16 ambaye wapalestina wanaamini alitekwa nyara na kuuwawa na jeshi la Israel.
Polisi bado wanachunguza iwapo mauaji yake ni kisa cha kulipiza kisasi kilichofanywa na waisraeli baada ya kutekwa nyara na kuuwawa vijana wake watatu, ambao miili yao ilipatikana katika Ukingo wa Magharibi.
Kwa upande mwengine kupitia taarifa yake, Wizara ya sheria nchini Israel imesema idara ya polisi imeanzisha uchunguzi juu ya tukio hilo.
Aidha msemaji wa polisi nchini Israel Micky Rosenfeld amesema Khdeir ni mmoja wa vijana sita waliokamatwa na kuzuiliwa, watatu kati yao walikutwa na visu.
Israel yasema imeanzisha uchunguzi ya kubainisha mauaji ya Khdeir
Siku ya Jumamosi ghasia zilitokea kati ya polisi na waandamanaji Jerusalem Mashari na katika vijiji vya kiarabu Kaskazini mwa Isarel huku Palestina ikisema kuwa kijana wao aliyeuwawa wiki hii alichomwa moto akiwa hai.
Kulingana na vyombo vya habari vya Palestina, uchunguzi uliofanywa kwa mwili wa Mohammed Hussein ulionyesha kwamba alichomwa moto mpaka akafa.
Athari katika mapafu yake na sehemu nyengine za ndani mwilini mwake zilionyesha kwamba alivuta hewa ya baruti wakati alipokuwa hai.
Mwili wake uliungua kwa asilimia 90 na pia kichwa chake kilionekana kugongwa na kitu. Uchunguzi huo ulifanywa na madaktari wote wa Israel na Palestina lakini bado mpaka sasa Israel haijatoa ripoti yake.
Roketi na mabomu yameendelea kurushwa kutoka Gaza hadi Kusini mwa Israel huku jeshi la Israel nalo likiendelea na mashambulizi yake ya angani dhidi ya mashambulizi yanayolengwa katika maeneo yake.
Waziri wa Usalama wa ndani wa Israel Yitzhak Aharonovitch amesema hakutakuwa na uvumilivu wa aina yoyoyte kwa wale watakaojaribu kuleta usumbufu, huku mkuu wa polisi Yohanan Danino akikiri kwamba hizi ni siku ngumu sana na kwamba vikosi vyake vinajaribu kudhibiti hali na kuzuwiya kusambaa kwa ghasia zaidi.
Mwandishi Amina Abubakar/Reuters/dpa
Mhariri Abdu Mtullya