Marekani yamuuwa aliyepanga shambulizi la Kabul
28 Agosti 2021Operesheni hiyo ya usiku wa kuamkia Jumamosi ilimlenga mtuhumiwa wa kundi la wanamgambo lenye mafungamano na lile linalojiita Dola la Kiislamu, IS-K kwenye jimbo la mashariki Nangahar. Msemaji wa Kamandi Kuu ya Marekani, Bill Urban amesema dalili za awali zinaonesha kuwa wamemuua mlengwa na hakuna raia wowote waliouawa.
Shambulizi hilo limefanyika baada ya Rais Joe Biden kuapa kupambana na IS baada ya mashambulizi ya Alhamisi yaliyosababisha mauwaji ya wanajeshi 13 wa Marekani na takriban raia 79 wa Afghanistan. IS ilikiri kuhusika na shambulizi, huku kundi la Taliban likikanusha kuhusika kwa namna yoyote ile. Biden pia aliliagiza jeshi kufanya mashambulizi dhidi ya viongozi wa IS, pamoja na mali za kundi hilo.
Ama kwa upande mwingine, Marekani imesema itaendelea kuwaondoa raia wa Afghanistan kutoka uwanja wa ndege wa Kabul hadi dakika ya mwisho, licha ya kuwepo wasiwasi kuhusu mashambulizi zaidi ya kundi la IS.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema bado kuna vitisho vya kuaminika katika uwanja huo wa ndege. Marekani bado inaendelea na mchakato wa kuwaondoa raia wa Afghanistan wanaotaka kuondoka. Aidha, msemaji wa kundi la Taliban amesema kwamba wamechukua udhibiti wa maeneo ya uwanja wa ndege. Hata hivyo, Marekani imekanusha taarifa hizo.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jen Psaki wataalamu wa usalama wa taifa wamesema kuna uwezekano wa kutokea shambulizi jingine na siku zijazo zitakuwa hatari zaidi. Siku ya mwisho ya vikosi vya Marekani kuondoka Afghanistan ni Agosti 31. Nchi nyingi za Jumuia ya Kujihami ya NATO zimemaliza safari zao za dharura za ndege kuwaondoa watu.
Marekani yawaondoa watu 105,000
Marekani pamoja na washirika wake wamewaondoa watu 12,500 kutoka uwanja wa ndege wa Kabul katika muda wa saa 24 zilizopita, licha ya ukweli kwamba operesheni ya kuwaondoa watu iliahirishwa kutokana na shambulizi hilo. Ikulu ya Marekani imesema watu 8,500 waliondolewa moja kwa moja na jeshi la Marekani na wengine 4,000 waliondolewa na ndege za washirika wake. Marekani imesema operesheni ya kuwaondoa watu imewajumuisha watu 105,000 hadi sasa.
Wakati huo huo, wanajeshi wote wa Ujerumani pamoja na maafisa waliokuwepo Afghanistan wamewasili Ujerumani. Ndege tatu za kikosi cha anga zilitua jana usiku katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Wunstorf karibu na Hanover. Ndege moja ya jeshi chapa ya Airbus A310 na ndege mbili za usafirishaji chapa A400M zilitumika kuwarudisha Ujerumani wanajeshi hao. Wanajeshi hao wamerejea nyumbani baada ya kukamilika kwa shughuli ya mwisho ya kuwaondoa nchini Afghanistan.
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Annegret Kramp-Karrenbauer alikuwemo pia ndani ya ndege mojawapo. Ndege hizo ziliondoka Tashkent, ngome iliyokuwa inatumiwa na jeshi la Ujerumani kwa ajili ya utaribu wakati wa operesheni ya kuwaondoa watu.
Kramp-Karrenbauer amesema operesheni ya kuwaondoa watu Kabul ilikuwa ya hatari. ''Jeshi la Ujerumani liliwaleta watu wengi lilivyoweza kwenye eneo salama, chini ya mazingira magumu sana,'' alifafanua Kramp-Karrenbauer.
Operesheni za Ujerumani na Ufaransa
Waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani amesema watu 5,347 kutoka takriban nchi 45 waliondolewa Afghanistan kwa kutumia ndege za kijeshi za ujerumani, wakiwemo raia 500 wa Ujerumani na zaidi ya 4,000 wa Afghanistan.
Kwa upande wake Ufaransa imesema imemaliza operesheni ya kuwaondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan. Waziri wa ulinzi Florence Parly amesema operesheni ya kuwaondoa watu ilisamama kwa sababu hapakuwa na mazingira ya kiusalama. Parly amesema Ufaransa itaendelea kuwasaidia wanaohitaji ulinzi wakati wa kuondoka Afghanistan. Amesema vikosi vya Ufaransa vilifanikiwa kuwaondoa Afghanistan zaidi ya watu 3,000 kabla ya shughuli hiyo kusitishwa.
(AP, DPA, AFP, Reuters)