1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yamuwekea Kony dola milioni 5

Admin.WagnerD4 Aprili 2013

Marekani imetangaza kitita cha dola milioni tano kwa atakayefanikisha kukamatwa kwa kiongozi wa kundi la waasi la Lord's Resistance Army LRA, la nchini Uganda, ambaye ni mmoja wa watu wanaotafutwa sana duniani.

https://p.dw.com/p/189g3
Kiongozi wa LRA, Joseph Kony
Kiongozi wa LRA, Joseph KonyPicha: STUART PRICE/AFP/Getty Images

Tangazo hilo la Marekani limekuja siku moja tu baada ya Uganda na Washington kusema kuwa wamelazimika kusitisha msako wa miaka miwili wa mbabe huyo wa kivita katika misitu ya Jamhuri ya Afrika ya kati, baada ya waasi kuipindua serikali.

ADDITION / BYLINE TO GO WITH AFP STORY BY MAX DELANEY Wanajeshi wa Uganda wakifanya doria katika misitu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, kumsaka Kony.
Wanajeshi wa Uganda wakifanya doria katika misitu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, kumsaka Kony.Picha: Yannick Tylle/AFP/Getty Images

Jina la Kony lilijumlishwa katika programu ya zawadi za uhalifu wa kivita ya wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, pamoja na wenzake kutoka kundi la LRA -Okot Odhiambo na Dominic Ongwen, na Sylvestre Madacumura kutoka kundi la waasi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda, FDLR, kwa matumaini kwamba watu hao watafikishwa mbele ya sheria, katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC ya mjini The Hague.

Hakamatwi kwa urahisi

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry, alisema vitendo vya utesaji na ugaidi vilivyofanywa na kundi la LRA kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 dhidi ya watoto nchini Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Jamhrui ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini lazima vikomeshwe. Lakini waziri huyo alikiri kuwa Kony na washirika wake hawatakamatwa kwa urahisi. Rais wa Marekani, Barack Obama, mwaka jana alirefusha muda wa operesheni ya wanajeshi 100 maalumu wa Marekani, ambayo ilizinduliwa mwaka 2011 kusaidiana na jeshi la Uganda kumsaka Kony katika misitu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, lakini hadi sasa hawajafanikiwa.

Uganda ilitangaza kusitisha operesheni ya kumsaka Kony katika Jamhuri ya Afrika ya kati baada ya waasi wa Seleka kutwaa madaraka, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la UPDF, Kanali Felix Kulaigye. Wakati hayo yakijiri, Jumuiya ka kiuchumi ya mataifa ya Afrika ya kati, ECCAS, imependekeza kuundwa kwa kamati itakayosimamia uchaguzi wa rais wa mpito katika Jamhuri ya Afrika ya kati kwa kipindi kisichozidi miezi 18. Mawaziri wa ECCAS pamoja na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya wamepanga kusafiri kwenda nchini humo kuwasilisha ujumbe huo kwa raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

lord resistance army.jpg Waasi wa LRA wakionekana wakati kiongozi wao Kony akikutana na maafisa wa serikali na wabunge wa Uganda na wawakilishi wa mashirika ya kiraia mwaka 2006.
Waasi wa LRA wakionekana wakati kiongozi wao Kony akikutana na maafisa wa serikali na wabunge wa Uganda na wawakilishi wa mashirika ya kiraia mwaka 2006.Picha: AP

Afrika Kusini kuondoa wanajeshi wake Afrika ya kati

Wakati huo huo, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, amesema nchi yake iko tayari kuondoa wanajeshi wake walioko Jamhuri ya Afrika ya Kati, uamuzi ambao utahitimisha makubaliano ya kijeshi kati ya mataifa hayo mawili, uliopelekea kuwekwa kituo cha kijeshi cha Afrika Kusini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Afrika Kusini imesema pia haiungi mkono kutwaa madaraka kwa nguvu, na Umoja wa Afrika umeisimamisha Jamhuri ya Afrika ya Kati uanachama, kufuatia hatua ya waasi wa Seleka kuchukua madaraka na kiongozi wao, Michel Djotodia, kujitangazia urais na kusitisha katiba.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,afpe

Mhariri: Josephat Nyiro Charo.