Marekani yanyoshewa kidole huko Davos katika mzozo wa fedha
29 Januari 2009Kikao hicho kinawaleta pamoja washiriki 2500 wakiwemo viongozi 40 wa serikali.Viongozi hao wawili waliinyoshea kidole Marekani kwa kuchangia pakubwa katika msukosuko wa fedha unaoendelea kote ulimwenguni.Waziri Mkuu wa Uchina Wen Jiabao alikuwa wa kwanza kupanda jukwaani na kauli zilizoishtumu Marekani kwa kulipa kipa umbele suala la kupata faida bila ya kujali athari zake.Baadhi ya sera za uchumi za nchi hiyo zililaumiwa kwa kutofanikisha hatua za kuchanga pesa na badala yake kuongeza viwango vya ununuzi.
Kwa upande mmoja Waziri Mkuu Wen Jiabao alishtumu ukuaji kwa kasi taasisi za fedha uliokuwa na lengo la kuimarisha viwango vya faida na kwa upande wa pili kutowajibika kwa taasisi za kusawazisha hali nzima.Kiongozi huyo aliongeza kuwa mparaganyiko huo umeiwia nchi yake vigumu inayohitaji uchumi wake kukua kwa asilimia 8 mwaka huu ndipo iweze kusawazisha mahitaji yake ya kijamii.Kulingana na tathmini ya Mfuko wa Fedha Ulimwenguni,IMF uchumi wa Uchina unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.7.Hata hivyo bwana Wen Jiabao ametoa wito wa marekebisho kufanyika kwa haraka katika taasisi za kimataifa za fedha ili kuokoa jahazi.
Punde baada ya kauli hizo Waziri Mkuu wa Urusi Vladimir Putin alichukua fursa hiyo na kuelezea mparaganyiko ulioko kuwa kama dhoruba iliyo na vyanzo vingi.''Tatizo hili lina vyanzo vingi….kuporomoka kwa mifumo ya fedha ya ulimwengu…..uongozi mbaya pamoja na udhibiti mdogo wa serikali vyote vimechangia
Bwana Putin alisisitiza kuwa azma yake haikuwa kuikosoa Marekani.Kiongozi huyo hakusita kutoa wito wa kuimarishwa kwa usalama katika sekta ya nishati na kwamba nchi yake ina azma ya kupanua wigo wa wateja wake wa nje.
Aligusia umuhimu wa kusawazisha bei ya nishati inayoenda sanjari na mahitaji.Hata hivyo Waziri Mkuu Vladimir Putin pamoja na mwenzake wa Uchina Wen Jiabao walitoa wito wa ushirikiano wa kimataifa katika juhudi za kulitafutia suala hilo ufumbuzi.
Wakati huohuo Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel na Mawaziri Wakuu wa Uingereza na Japan,Gordon Brown na Taro Aso wanatarajiwa kuhutubia kikao hicho cha Davos wiki hii.Itakumbukwa kuwa viongozi hao wawili tayari wameidhinisha mipango inayogharimu mabilioni ya dola kupambana na tatizo hilo la kiuchumi.
Hatua hizo zimezua mitazamo tofauti hata katika sekta ya biashara kama anavyoeleza Rupert Madoch mmiliki wa Shirika la Habari la News Corp.Anaeleza kwamba masoko huria ni msingi muhimu katika biashara.''Tusipoteze mwelekeo wa kuelewa chanzo cha kuzalisha fedha ulimwenguni….Masoko huria….ubepari …hilo limethibitishwa kila wakati.Ukilinganisha masoko huria na masoko yasiyokuwa huria utaona kwamba masoko huria ndiyo chachu ya mafanikio kila wakati.
Kwa upande mwengine mashirika ya misaada yanatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuongeza viwango vya ufadhili ili kuzisaidia nchi masikini kupambana na uhaba wa chakula katika kipindi hiki kigumu cha kiuchumi.Hali hiyo imesababishwa na ongezeko la bei za vyakula.Tathmini zinaonyesha kuwa bei za vyakula zimepungua ikilinganishwa na viwango vya mwaka uliopita ila bado raia katika mataifa mengi yanayoendelea yanakabiliwa na uhaba wa chakula na tishio la njaa.
RTRE
DPAE