Marekani yaongoza vifo vya COVID-19 duniani
12 Aprili 2020Kulingana na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, mripuko huo umeshasabbaisha vifo 20,506 nchini Marekani na taifa hilo pia linaongoza kwa visa vya maambukizi ya virusi vya corona vilivyopindukia 527,111.
Italia, taifa lililoathiriwa vibaya barani Ulaya, limerikodi vifo 19,468 vilivyotokana na ugonjwa wa COVID-19.
Hata hivyo, matumaini yameanza kupanda kwenye mataifa ya Ulaya Magharibi na katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi nchini Marekani kuwa sasa mripuko huo unaelekea kufikia kilele chake.
Wengi wanatizama mfano wa mji wa Wuhan - mji wa katikati ya China ambao ndiyo kitovu cha virusi vya corona - ambako maafisa wa serikali wameanza kuondoa vizuizi na shughuli za kawaida zimeanza kurejea.
Makanisa yanatarjiwa kuwa matupu leo wakati wa ibada ya sikukuu ya Pasaka baada ya mikusanyiko muhimu kupigwa marufuku kutokana na virusi vya corona ambavyo hadi leo Jumapili maambukizi yake yamepindukia milioni 1.7 kote duniani.
Virusi hivyo tayari pia vimesababsiha vifo vya zaidi ya watu 107,000 tangu vilipozuka kwa mara ya kwanza nchini China, Disemba iliyopita.
Dalili njema zimeanza kuonekana
Lakini ishara za kupungua maambukizi ya idadi ya vifo katika mataifa kadhaa ya Ulaya na kitovu cha ugonjwa huo nchini Marekani zinatia moyo.
Takwimu za siku ya Jumamosi kutoka Uhispania zimeongeza matumaini baada ya taifa hilo kurikodi vifo 510, ambapo idadi ilishuka kwa siku tatu mfululizo.
Idadi ya watu waliokufa kutokana na COVID-19 nchini Ufaransa imepungua kwa theluthi kuanzia Ijumaa hadi vifo 635 siku ya Jumamosi.
''Inaonesha mripuko huu umefikia kilele lakini bado upo. Tunapaswa kuendelea kuwa thabiti,'' alisema Jerome Salomon, afisa wa afya nchini Ufaransa.
Italia imesema idadi ya vifo nchini humo imeendelea kupungua lakini serikali imekataa msukumo wa kuondoa vizuizi na kurefusha marufuku zilizopo hadi Mei 3.
Miji ya New York na New Orleans nchini Marekani imeshuhudia kupungua kwa idadi ya maambukizi, vifo na watu wanalazwa hospitali.
Uingereza hali bado ni mbaya
Lakini siku ya Jumamosi, Uingereza ilirikodi siku ya pili ya idadi kubwa ya vifo wakati Waziri Mkuu Boris Johnson akiendelea kupata nafuu baada ya kupata maambukizi ya COVID-19
Ingawa maambukizi ulimwenguni yamepindukia milioni 1.7, idadi kamili inadhaniwa kuwa kubwa zaidi kwa kuwa mataifa mengi yanawapima watu walioonesha dalili pekee.
Wataalamu wengi wa afya na Shirika la Afya Duniani (WHO) wametahadharisha dhidi ya mataifa kuchukua hatua za kuondoa marufuku zilizowekwa.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Ghebreyesus, alionya siku ya Ijumaa kuharakisha kuondoa vizuizi vilivyopo kunatishia kuzuka upya kwa wimbi jingi la maambukizi ya virusi vya corona.
Mwandishi: Rashid Chilumba/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef