1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaombwa kutojiondoa katika makubaliano ya nyuklia

Yusra Buwayhid
20 Aprili 2018

Wabunge wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wamelionya Baraza la Congress la Marekani juu ya uharibifu utakaotokea iwapo Marekani itajiondoa katika makubaliano ya Iran ya kupunguza silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/2wNOx
Österreich Wien Atom Verhandlungen
Picha: Getty Images/AFP/J. Klamar

Wabunge wapatao 500 kutoka Uingereza, Ufaransa na Ujerumani Alhamis wamelisisitiza Baraza la Congress la Marekani kuyanusuru makubaliano ya silaha za nyuklia ya Iran kabla ya Marekani kujiondoa mwezi ujao.

Utawala wa Rais Donald Trump umetaka makubaliano hayo ya silaha za nyuklia yafanyiwe marekebisho ifikapo Mei 12, venginevyo itaiwekea tena vikwazo Iran na kuyavuruga makubaliano hayo yaliyofikiwa 2015 kati ya Iran na nchi sita za Russia, Ufaransa, Uingereza, China, Marekani na Ujerumani.

Marekani inatarajia kufikia makubaliano na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani katika kushughulikia wasiwasi wa ulionao kuhusu makubaliano ya nyuklia na Iran, amesema balozi wa Marekani anaehusika na upunguzaji wa nguvu za silaha, Robert Wood, katika mkutano na waandishi habari mjini Geneva, Aprili 19.

Wood ameeleza kwamba majadiliano ni makali kuelekea siku ya mwisho iliyopangwa ya Mei 12, na kwamba Marekani ina wasiwasi juu ya kushindwa kushughulikia mpango wa makombora wa Iran, wenye muda wa miaka 10 pamoja na hatua za Iran kwa jumla katika kanda ya Mashariki ya Kati.

Wood amesema Marekani inamatumaini kwamba majadiliano na washirika wake wa nchi za Ulaya yatazaa matunda ambayo yatamridhisha rais wa Marekani Donald Trump.

"Kuhusu suala la Iran, tushasema na rais keshaliweka wazi hilo. Uamuzi utahitajika kuchukuliwa ifikapo Mei 12 kuhusu mustakbali wa Marekani na kushiriki kwake katika JCPOA," amesema Wood katika mkutano huo na waandishi habari.

Kujiondoa katika makubaliano kutakuwa chanzo cha migogoro Mashariki ya Kati

Iran imesema itaendelea kuheshimu Mpango wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA) kama nchi nyingine husika nazo zitafanya hivyo, na itaachana na makubaliano hayo pale Marekani itakapojiondoa.

Iran Atomabkommen
Barua hiyo imesema Marekani inataka kujiondoa katika mpango wa nyuklia licha ya Iran kutimiza majukumu yake.Picha: picture-alliance/epa/D. Calma

Wabunge kutoka nchi tatu za Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumaji ambazo ziliweka saini katika mkataba huo, walionya kwamba kuachana na mkataba ni kukosa udhibiti juu ya mpango wa nyuklia wa Iran na hilo linaweza kuwa chanzo cha migogoro katika Mashariki ya Kati.

Katika barua yao iliochapishwa katika magazeti makubwa Alhamis na Ijumaa, wabunge hao wamesema miaka kumi na tatu ya mazungumzo na Iran imeiwezesha jumuiya ya kimataifa kulazimisha kufanywa uchunguzi ambao haukuwahi kufanywa dhidi ya mpango wa kinyuklia wa Iran, kuondosha vifaa vingi vya uimarishaji wa silaha za nyuklia katika mitambo yake, na hatimaye kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya silaha za nyuklia bila ya hata tone moja ya damu kumwagwa.

"Kujiondoa kwa Marekani, kutaharibu uaminifu wetu kama washirika wa kimataifa katika mazungumzo, na kwa ujumla katika uuwanja wa kidiplomasia tutapoteza uaminifu kama chombo cha kufikia amani na kuhakikisha usalama,"imeeleza barua hiyo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wataelekea mjini Washington wiki ijayo kuushinikiza utawala wa Trump kubakia ndani ya makubaliano hayo.

Mwandishi: Yusra Buwahyid

Mhariri: Caro Robi