Marekani yapendekeza vikwazo vya silaha kwa Sudani Kusini
18 Novemba 2016Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power amesema kuwa rasimu ya maazimio itawasilishwa katika baraza hilo katika siku sijazo. Azimio hilo likiwa na lengo la kuzuia uuzwaji wa silaha katika nchi hiyo ya Afrika, na pia kuiwekea vikwazo hatua ambayo inaweza kuzua mgogoro na Urusi nchi ambayo inapinga vikwazo vya silaha kwa nchi hiyo.
Sudan Kusini ni nchi ambayo iko katika hatua ya kuporomoka alisema Power na kuongeza kuwa katika siku zijizo Marekani itawasilisha pendekezo la vikwazo vya silaha na kulazimisha vikwazo kuwalenga wanasiasa ambao wamekuwa kizingiti kikubwa cha kupatikana kwa amani nchini humo.
Katika nchi wanachama wenye haki ya kupiga kura ya turufu, Uingereza na Ufaransa zimeunga mkono, wakati Urusi imepinga na China imejiuzia kusema chochote kwa sasa.
Hatua hiyo inafuatia ripoti ya hivi karibuni ambayo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ambaye alionya kuwa Sudan Kusini inakabiliwa na hatari ya kuingia katika matataizo makubwa na kuwa vikosi vya wanajeshi wa kulinda amani 14,000 waliopelekwa nchini humo havina nguvu na uwezo wa kuzuia uhalifu huo ikiwa utatokea.
Pendekezo hilo la Marekani ambalo limeshuhudiwa na shirika la habari la Ufaransa AFP linahimiza mwaka mmoja wa zuio la kuuza silaha, risasi, magari ya kivita pamoja na vifaa vingine.
Naibu Balozi wa Urusi, Petr Iliichev amekosoa pendekezo hilo na kusema kuwa ni mapema sana na linaweza kuwa vigumu vikwazo hivyo kusaidia kutatua mgogoro, huku akionya vikwazo dhidi ya viongozi wa Sudan Kusini ni kiwango kikubwa cha kutokuwajibika.
Akiilenga Mrekani alisema kuwa Salva Kiir ni mlengwa ambaye anatarajiwa kufuata kile kilichotokea kwa Muamar Gaddafi aliyekuwa kiongozi wa Libya aliyepinduliwa mwaka 2011. Naye naibu balozi wa China, Wu Haito amesema kuwa baraza hilo linatakiwa kijiepusha na masuala ya vikwazo ili kuepusha hali kuwa mbaya zaidi.
Baada ya kurejea katika ziara yake nchini Sudan Kusini, Adama Dieng mshauri maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya halaiki anasema kuwa aliona ishara zote za kuwepo kwa chuki za kikabila ambazo zinawalenga raia na kuwa kama hakutachukuliwa hatua za mapema kuna uwezekano mkubwa wa kutokea kwa mauaji ya halaiki.
Mwandishi: Celina Mwakabwale AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo