Marekani yapiga marufuku raia wake kwenda Korea kaskazini
1 Septemba 2017Wakati huo huo waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa amesema Korea kaskazini ina uwezo wa kurusha makombora ya masafa marefu katika miezi michache ijayo na kuitaka China kuchukua hatua zaidi kutatua mzozo huo.
Hatua ya kupiga marufuku raia wa marekani kutembelea Korea kaskazini imechukuliwa kutokana na kifo cha mwanafunzi Otto Warmbier mwezi Juni, siku chache baada ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 22 kurejeshwa nyumbani akiwa hajitambua kufuatia kufungwa jela kwa zaidi ya mwezi mmoka nchini humo.
Alihukumiwea kwa kosa la kula njama dhidi ya taifa hilo kwa kujaribu kuiba bango la propaganda kutoka katika hoteli mjini Pyongyang na kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 na kazi ngumu, huku rais Donald Trump akiulaumu utawala wa kinyama wa Pyonyang , kwa hali madhara aliyoyapata.
Katika tovuti yake , wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imesema imechukua uamuzi huo kutokana na "hali mbaya na kitisho kinachoongezeka cha kukamatwa na kufungwa kwa kipindi kirefu raia wa Marekani".
Wamarekani watatu wanaoshutumiwa kwa uhalifu mbali mbali dhidi ya taifa hilo wako jela nchini Korea kaskazini, nchi ambayo imo katika hali ya mvutano na wasi wasi mkubwa na utawala wa Trump kuhusiana na mpango wake uliopigwa marufuku wa silaha za kinyuklia.
Mapema wiki hii Pyongyang ilifyatua kombora kupitia anga ya Japan , katika hatua ya juu kabisa ya kuchochea mzozo huo, na imetishia kurusha makombora zaidi kuelekea kisiwa cha Guam ambacho kinamilikiwa na Marekani katika bahari ya Pasifiki.
Majaribio ya Korea kaskazini
Mwezi Julai Korea kaskazini ilifanya majaribio yake mawili yaliyofanikiwa ya makombora ambayo yana uwezo wa kuruka kutoka bara moja kwenda lingine, na hatimaye kuweza kufika nchini Marekani.
Marufuku hiyo hata hivyo haiwagusi waandishi habari, wawakilishi wa shirika la msalaba mwekundu, wale wanaosafiri kwa madhumuni ya kutoa msaada wa kiutu , ama safari ambazo wizara ya mambo ya kigeni inaziona kuwa na maslahi na Marekani. Lakini asasi za kijamii zinazofanyakazi nchini Korea kaskazini kibinafsi zimeeleza wasi wasi wake juu ya vipi hatua hiyo itafanyakazi na athari zake katika kazi yao.
Raia wachache wa Marekani ambao wamebaki nchini humo wameondoka siku ya Alhamis, zimesema baadhi ya ripoti. Waziri anayehusika na kuziunganisha Korea mbili wa Korea kusini Lee Eugene amesema Korea kaskazini inapaswa kuacha uchokozi.
"Korea kaskazini inaendelea kufanya uchokozi. Msimamo wa serikali yetu kwamba tunahitaji suluhisho la amani katika suala la kinyuklia la Korea kaskazini na rasi ya Korea haujabadilika. Pia , tunaitaka Korea kaskazini kuacha kutoa matamshi ya ukosoaji na vitisho na kuchukua njia ya mazungumzo na ushirikiano."
Wakati huo huo waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amekiambia kituo cha redio cha RTL kwamba hali ni mbaya , tunaona Korea kaskazini ikiwekea malengo ya kesho ama kesho kutwa kurusha makombora yenye vichwa vya kinyuklia. Kwa wakati huu ambapo Korea ya kaskazini ina uwezo wa kushambulia Marekani , hata Ulaya, lakini hasa Japan na China, hali itakuwa mbaya zaidi.
Le Drian ambae alizungumza na mwenzake wa China siku ya Alhamis , amesema kila kitu kinapaswa kufanywa kuhakikisha vikwazo vya hivi karibuni vya umoja wa Mataifa vinatekelezwa na kuitaka China , mshiriam mkubwa wa kibiashara wa Pyonyang, kuchukua juhudi zote kuvitekeleza.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Idd Ssessanga