Marekani yashutumu majasusi wa Urusi kudukua uchaguzi 2016
14 Julai 2018Hizi ni shutuma za kwanza za kina kuwahi kufanyika katika madai ya muda mrefu kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa rais kumsaidia mgombea wa chama cha Republican Donald Trump.
Mashitaka hayo, ambayo ni madai ya kula njama katika maeneo kadhaa yanayohusu udukuzi wa hali ya juu na utoaji wa nyaraka , unazusha hali ya wasi wasi kwa ajili ya mkutano wa kilele wiki ijayo baina ya marais Trump na Vladimir Putin.
Maafisa wa idara ya ujasusi katika jeshi la Urusi, inayojulikana kama GRU, kwa chini chini walikuwa wakichunguza kompyuta za kampeni ya mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton pamoja na kamati ya kampeni ya chama cha Democratic, na kuiba idadi kubwa ya data, mashitaka hayo yamesema.
"Pamoja na kutoa nyaraka moja kwa moja kwa umma, washitakiwa walihamisha nyaraka zilizoibiwa kwenda katika shirika lingine, ambalo halikutajwa katika mashitaka hayo, na kujadili muda wa kutoa nyaraka hizo katika juhudi za kuongeza athari katika uchaguzi huo," Naibu mwanasheria mkuu wa serikali ya Marekani Rod Rosenstein aliwaambia waandishi habari.
Kushitakiwa kwa watu hao jana Ijumaa (13.07.2018) kumekamilishwa na mshauri maalum Robert Mueller kama sehemu ya uchunguzi wake kuhusiana na uhusika wa Urusi katika uchaguzi huo. Alikuwa kwanza Mueller ambaye moja kwa moja aliishitaki serikali ya Urusi kwa kuingilia uchaguzi, ambao bila kutarajiwa Trump alishinda. Serikali ya Urusi inakana kuingilia kati huko.
Trump afahamishwa
Rosenstein alisema alimfahamisha rais Trump mapema wiki hii juu ya mashitakam hayo. Hayana madai kwamba raia wa Marekani walifanya uhalifu, alisema.
Masaa machache kabla ya mashitaka hayo kutangazwa, Trump aliuita uchunguzi huo wa Mueller "utafutaji mchawi ulioghushiwa" ambao unaathiri uhusiano kati ya Marekani na Urusi.
Tangazo hilo la mashitaka limekuja katika wakati mbaya kwa Trump, ambaye alikutana na malkia Elizabeth katika kasri la Windsor jana Ijumaa na kunywa nae chai wakati wa ziara yake nchini Uingereza.
Trump alisema , bila shaka atamuuliza Putin juu ya kuingilia wakati watakapokutana katika mkutano uliopangwa kufanyika mjini Helsinki siku ya Jumatatu.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi ilisema jana Ijumaa kwamba mashitaka hayo yana lenga katika kuharibu hali ya hewa kabla ya mkutano huo wa kilele. Imesema hakuna ushahidi kwamba watu hao 12 walioshitakiwa wanahusika na ujasusi katika jeshi ama udukuzi.
Trump atakiwa kufuta mkutano
Wabunge kadhaa maarufu wa chama cha Democratic walimtaka Trump kufuta mkutano wake na Putin.
"Kutokana na mashitaka haya yaliyotolewa na idara ya sheria kwamba Warusi hawa walikula njama kushambulia demokrasia yetu na walikuwa wanawasiliana na Wamarekani kuingilia kati uchaguzi wetu, rais Trump anapaswa bila kusita kufuta mkutano wake na Vladimir Putin," alisema seneta Jack Reed, seneta wa ngazi ya juu wa chama cha Democratic katika kamati ya huduma za jeshi katika baraza la seneti.
Mueller anachunguza iwapo kampeni ya Trump ilishirikiana na Urusi na iwapo rais alitafuta kwa njia ambayo ni kinyume na sheria kuzuwia uchunguzi dhidi ya Urusi.
Mashirika ya ujasusi ya Marekani yalifikia hitimisho Januari mwaka 2017 kwamba Urusi, ilifanya juhudi zilizoamrishwa na rais Putin, kutumia propaganda na udukuzi kuingilia kati uchaguzi kumuathiri Clinton na hatimaye kumsaidia Trump kushinda.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Caro Robi