1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yataka Ukraine isaidiwe na silaha zaidi

15 Juni 2023

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin Alhamis mjini Brussels, amewataka marafiki wa Ukraine kuisaidia na silaha zaidi za kupambana na uvamizi wa Urusi.

https://p.dw.com/p/4SdMF
Belgien NATO Verteidigungsminister Treffen Brüssel | Stoltenberg, Milley, Austin und Reznikov
Picha: Yves Herman/REUTERS

Austin amesema msaada zaidi unaohitajika ni mifumo ya angani ya kujilinda.

Akihutubia mkutano wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO yenye takribani nchi 30 wanachama na inayoongozwa na Marekani, waziri huyo wa ulinzi amesisitiza kwamba Ukraine inahitaji misaada ya muda mfupi na muda mrefu, kwa kuwa vita vya Ukraine vitadumu kwa muda mrefu.

Austin amesema NATO tayari imeshaisaidia Ukraine na mifumo ya kujilinda ya Patriot, IRIS-T na NASAMS iliyoisaidia nchi hiyo kujilinda kutokana na makombora ya Urusi, ila ameongeza kwamba misaada mingi zaidi inahitajika.

"Dhamira yetu kwa Ukraine ni ya muda mrefu na jumuiya hii inasalia pamoja. Juhudi zetu zinatokana na msingi wa mkakati wa muda mrefu na tunataka kuhakikisha kwamba, Ukraine, ina uwezo inaohitaji wa kuwalinda raia wake na mipaka yake, kuzuia uchokozi zaidi kutoka kwa Warusi na hatimaye kupata ushindi dhidi ya kampeni ya kinyama na ya unyakuzi ya Putin," alisema Austin.

NATO Treffen der Verteidigungsminister zum Ukraine Krieg
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd AustinPicha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

Vita vya nyuklia havistahili kuanzishwa

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, amesema jumuiya hiyo haioni dalili zozote kwamba Urusi imebadili msimamo wake wa silaha za nyuklia. Hii ni baada ya Rais wa Belarus Alexander Lukashenko kudai kwamba nchi yake tayari imepokea silaha za kimkakati za nyuklia kutoka Moscow.

Stoltenberg amesema Urusi inastahili kufahamu kwamba vita vya nyuklia haviwezi kushindwa na yeyote kwa hiyo havistahili kupiganwa. Stoltenberg vile vile ameongeza kuwa madhumuni ya mkutano huo wa NATO ni kuhakikisha kwamba Ukraine ina silaha za kutosha.

Hatua ya Urusi kupeleka silaha za nyuklia kwa mwandani wake Belarus inaonekana pakubwa kama onyo kwa nchi za Magharibi, wakati ambapo zinaongeza usaidizi wake wa kijeshi kwa Ukraine.

Waziri wa ulinzi wa Denmark, Troels Lund Poulsen naye ameainisha mipango ya uwezekano wa kuwapa mafunzo kwa kutumia ndege za kisasa, marubani wa ndege za kivita za Ukraine. Poulsen amesema mafunzo hayo yatafanyika nchini Denmark.

Mkutano huo lakini umefunikwa na kiwingu cha Uturuki kuikatalia Sweden kujiunga na jumuiya hiyo. Sweden inatarajia kuwa mwanachama wa NATO pale mkutano wa viongozi wa jumuiya hiyo utakapofanyika mjini Vilnius huko Lithuania mwezi ujao, ila uwezekano unaonekana kuwa mdogo kwa kuwa ni sharti kila mwanachama akubali kujiunga kwa mwanachama mpya.

Muhula wa Stoltenberg kufika mwisho

Hayo yakiarifiwa Stoltenberg amesema wanachama wa NATO ndio watakaoamua iwapo watataka aendelee kuhudumu kama Katibu Mkuu au watatafuta mrithi wake, baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka tisa.

Belgien NATO Verteidigungsminister Treffen Brüssel | Milley, Stoltenberg, Reznikov, und Austin
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg (kushoto) na Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Oleksiy ReznikovPicha: Simon Wohlfahrt/AFP/Getty Images

Kwa sasa nchi za NATO ziko katika harakati za kumtafuta atakayeichukua nafasi ya Stoltenberg kuelekea huo mkutano wa Vilnius.

Tayari muhula wa Stoltenberg mwenye umri wa miaka 64, ulikuwa umeongezwa kwa mwaka mmoja hadi Oktoba, kufuatia hatua ya Urusi kuivamia Ukraine.

Chanzo: DPA/AP/AFP/Reuters