Marekani yatakiwa kusitisha shughuli za kijeshi nchini Chad
20 Aprili 2024Katika barua iliowasilishwa kwa Waziri wa ulinzi wa Chad, mkuu wa jeshi la anga katika taifa hilo Idriss Amine Ahmed amesema amemtaka mwambata wa kijeshi wa Marekanikusitisha shughuli kwenye kituo hicho cha wanaanga kwa sababu imeshindwa kutoa nyaraka za kuhalalisha uwepo wao.
Msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani amesema mataifa hayo mawili yapo katika mazungumzo, kuhusu mustakabali wa ushirikiano wao katika masuala ya usalama.
Soma pia:Chad iko katika hali ya tahadhari baada ya shambulizi kwenye idara ya usalama
Marekani inao wanajeshi wapatao 100 nchini Chad, ambao wanahudumu kwa kupokezana zamu. Mkoloni wa zamani wa Chad, Ufaransa, inao wanajeshi 1000 na ndege za kivita katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati.
Hadi sasa Chad haijachukua hatua kama mataifa mengine yanayotawaliwa kijeshi ya Burkina Faso, Mali na Niger katika kusitisha ushirikiano wa kijeshi na Ufaransa na mataifa mengine ya Magharibi.