Marekani yatangaza msaada wa dola milioni 400 kwa Ukraine
21 Oktoba 2024Ziara hiyo ya Austin ambayo ni ya nne nchini Ukraine na labda ya mwisho kama waziri wa ulinzi wa Marekani, ilitarajiwa kuangazia juhudi za Marekani za kuisaidia Ukraine kuimarisha ulinzi wake wakati vikosi vya Urusi vikipiga hatua mashariki mwa nchi hiyo.
Austin amuhakikishia Zelensky mwendelezo wa msaada wa Marekani
Wakati wa mkutano wake na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Austin alimhakikishia kuhusu mwendelezo wa msaada wa Marekani kwa taifa hilo.
Ziara ya Austin inakuja kabla ya uchaguzi wa urais wa Marekani wa Novemba 5 ambapo rais wa zamani Donald Trump anagombea dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Democratic Kamala Harris.
Marekani yaondoa wazo la Ukraine kutumia silaha za masafa marefu
Trump ameashiria kusita kuendeleza msaada huo kwa Ukraine hatua ambayo huenda ikainyima Ukraine mfadhili wake mkubwa wa kijeshi na kifedha.
Hata hivyo Austin amepuuzilia mbali wasiwasi huo.
Rais Putin akutana na mwenzake wa UAE Zayed Al Nahyan
Rais wa Urusi Vladimir Putin alikutana jana na mwenzake wa Umoja wa Falme za kiarabu Mohammed bin Zayed Al Nahyan mjini Moscow, kwa mazungumzo yalioendelea hadi usiku wa manane kuamkia leo.
Kupitia mfasiri,Sheikh Mohammed alimuambia Putin kwamba wanaendelea kuongeza juhudi za kusimamia ubadilishanaji wa wafungwa na kwamba Umoja huo wa Falme za Kiarabu uko tayari kwa juhudi za ziada kutatua mizozo katika njia inayoshughulikia maslahi ya pande zote na kuunga mkono amani duniani.
Awali, Putin alikuwa amewapongeza Sheikh Mohammed na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kwa juhudi za upatanishi kuhusu Ukraine.
Mbali na hayo, wakati wa mkutano na balozi wa Urusi Georgy Zinoviev, naibu waziri wa mambo ya nje wa Korea KusiniKim Hong Kyun, alilaani hatua ya Korea Kaskazini ya kupeleka vikosi vyake Urusi na kusema inasababisha tishio kubwa la usalama kwa Korea Kusini na jamii ya kimataifa.
Haya ni kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wizara ya mambo ya nje ya Korea Kusini.
Urusi yasema ushirikiano na Pyongyang haulengi Korea Kusini.
Hata hivyo Ubalozi wa Urusi umemnukuu Zinoviev akisema ushirikiano wa Urusi na Pyongyang haulengi maslahi ya usalama ya Korea Kusini.
Katika mazungumo na katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO Mark Rutte hii leo, Rais wa Korea KusiniYoon Suk Yeol, amesema nchi yake haitakaa kimya kuhusiana na ushirikiano huo wa kijeshi.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Rutte amesema uwezekano wa Korea Kaskazini kupigana pamoja na Urusi katika vita vyake utasababisha kutanuka kwa vita hivyo.