Vikwazo dhidi ya wanaojaribu kuipindua serikali ya DRC
26 Julai 2024Katika taarifa yake, wizara ya fedha ya Marekani imesema muungano wa Mto Kongo, unaojulikana kwa jina la Kifaransa la "Alliance Fleuve Congo" (AFC), umekuwa ukichochea ukosefu wa utulivu wa kisiasa, migogoro na kusababisha watu kuyakimbia makaazi yao.
Moja ya mwanachama wa muungano wa AFC ni kundi la M23 linaloshtumiwa kwa kuwa na "historia ndefu" ya kuendesha uasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Soma pia: Kesi dhidi ya wanachama wa kundi la M23 yaanza
Miongoni mwa waliowekewa vikwazo ni kiongozi wa M23 Bertrand Bisimwa na Charles Sematama, kamanda wa kundi la Twirwaneho lenye mafungamano na muungano wa AFC linaloendesha oparesheni zake mashariki mwa Kongo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Mathew Miller kupitia taarifa ameeleza kuwa, AFC na washirika wake wana nia ya kuipindua serikali ya Kongo na wametumia vurugu kufikia malengo yao.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa vitendo vyao vimesababisha ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa na kuzidisha mzozo wa kibinadamu mashariki mwa Kongo.