1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatangaza zawadi nono kwa taarifa juu ya Al-Shabab

15 Novemba 2022

Marekani imesema itatoa zawadi ya hadi dola milioni 10 kwa yeyote ambaye atakuwa na taarifa kuhusu viongozi wakuu wa Al-Shabab.

https://p.dw.com/p/4JWUP
Somalia Militants Twitter
Picha: picture alliance / AP Photo

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeeleza kuwa, kwa mara ya kwanza itatoa donge nono kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa itakayowezesha kusaidia kutatiza mifumo ya kifedha ya kundi la Al-Shabab lenye mafungamano na Al-Qaeda.

Hivi karibuni wapiganaji wa Al-Shabab wameongeza mashambulizi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na maeneo mengine ya nchi hiyo kufuatia mashambulizi dhidi ya kundi hilo yanayofanywa na serikali mpya ya Rais Hassan Sheikh Mohamud.

Marekani imetangaza zawadi nono ya hadi dola milioni 10 kila mmoja kwa taarifa zozote juu ya maficho ya kiongozi wa Al-Shabab Ahmed Diriye, naibu wake Mahad Karate na Jehada Mostafa, raia wa Marekani anayesemakana kuwa na majukumu mbalimbali katika kundi hilo.

Soma pia: Jeshi la Somalia lawaua wapiganaji 20 Al Shabaab

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani inamhusisha Diriye na shambulio la mwaka 2020 katika kambi ya jeshi nchini Kenya, lililomuua mwanajeshi mmoja wa Marekani pamoja na wakandarasi wawili. Awali, Marekani ilitoa zawadi ya hadi dola milioni 6 kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu Diriye, ambaye pia anajulikana kama Abu Ubaidah.

Kwa mujibu wa bango lililotolewa na Marekani likiwa na picha za watatu hao, Washington imesema viongozi hao wa Al-Shabab wamehusika na mashambulizi mengi ya kigaidi nchini Somalia, Kenya na mataifa jirani na kusababisha vifo vya maelfu ya watu wakiwemo raia wa Marekani.

UN: Zaidi ya raia 600 wameuawa mwaka huu katika mashambulizi ya Al-Shabab.

Schweiz Genf | Amtsantritt Volker Türk, UN-Hochkommissar für Menschenrechte
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker TurkPicha: Salvatore Di Nolfi/REUTERS

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Turk alisema jana Jumatatu kuwa zaidi ya raia 600 wameuawa mwaka huu katika mashambulizi ambayo kwa kiasi kikubwa yamefanywa na Al-Shabab. Kulingana na takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa, takriban watu 613 wameuawa na wengine 948 wamejeruhiwa mwaka huu, idadi hiyo ikiwa ni ya juu zaidi tangu mwaka 2017 ikiashiria ongezeko la asilimia 30 kutoka mwaka uliopita.

Umoja wa Mataifa umeendelea kueleza kuwa, katika shambulio baya zaidi kuwahi kutokea katika muda wa miaka mitano, mashambulizi mawili ya mabomu yaliyodaiwa kufanywa na Al-Shabab mnamo Oktoba 29 yaligharimu maisha ya watu 121 na kuwajeruhi wengine 333 mjini Mogadishu.

Soma pia:Rais mpya wa Somalia aapa kukabiliana na ugaidi

Kundi hilo, ambalo liliwekwa kwenye orodha ya magundi ya kigaidi na Marekani mnamo mwezi Machi mwaka 2008, limekuwa likipambana kuipindua serikali dhaifu inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi kwa takriban miaka 15.

Rais Hassan Sheikh Mohamud, aliyeingia madarakani mwezi Mei, ameahidi kupambana na kundi hilo, huku wanajeshi wa serikali wakionekana kupata mafanikio katika uwanja wa mapambano dhidi ya Al-Shabab katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, kwa kuchukua udhibiti wa maeneo yaliyokuwa mikononi mwa kundi hilo kwa muda mrefu.

Mnamo mwezI Mei, Rais wa Marekani Joe Biden aliamua kutuma tena wanajeshi wa Marekani nchini Somalia, akiidhinisha ombi kutoka wizara ya ulinzi ya nchi hiyo, Pentagon, ambayo iliuona mfumo wa kupokezana uliopendelewa na mtangulizi wake Donald Trump kuwa hatari na usiokuwa na faida.

Rais Donald Trump aliwaondoa wanajeshi hao mnamo Desemba 2020, na kuwaacha wakiingia na kutoka kwa kazi maalumu kutokea nchi jirani ya Kenya, hatua ambayo wataalam walielezea kuwa ya gharama kubwa na hatari.