Marekani yatiwa wasiwasi na ushawishi wa China barani Afrika
14 Desemba 2022Wajumbe kutoka nchi 49 na Umoja wa Afrika ikiwa ni pamoja na viongozi 45 wa mataifa ya Afrika wanashiriki mkutano wa siku tatu kati ya Marekani na Afrika.Mkutano huo ulianza jana Jumanne na unafanyika mjini Washington Marekani.
Mkutano huu kati ya Marekani na Afrika ni wa aina yake kuwahi kufanyika tangu mwaka 2014 na rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kutangaza kuunga mkono Jumuiya ya Umoja wa Afrika kujumuishwa kwenye kundi la nchi tajiri na zile zinazoinukia kiuchumi la G20 kama mwanachama wa kudumu.
soma piaKwanini bara la Afrika ni muhimu kimkakati ?
Hatua hii inakuja baada ya mwenyekiti wa Umoja huo na rais wa Senegal Macky Sall na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kutowa ombi hilo. Afrika Kusini ni nchi pekee kutoka barani Afrika ambayo ni mwanachama wa kundi la G20 japo Umoja wa Afrika unajumuisha nchi 55 wanachama.
Vile vile Biden anatarajiwa kuunga mkono suala la usalama wa chakula na mabadiliko ya tabia nchi.Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken,nchi hiyo itatangaza mipango kadhaa ya uwekezaji utakaotowa fursa ya miradi ya ubadilishanaji mafunzo kwa wanafunzi kutoka Afrika pamoja na kusaidia wafanyabiashara wa bara hilo na bishara ndogondogo.
"Miradi hii inasimamia lengo moja, kuendelea kujenga ushirikiano wetu ili tuweze kwa ufanisi kuzishughulikia changamoto zetu tunazokabiliana nazo.Na hatimae tunaweza kujenga mustakabali wenye usalama,uhakika zaidi na wenye mafanikio kwetu wetu sote''
Ama kwa upande mwingine Marekani imeitahadharisha Afrika kwamba China na Urusi zinavuruga uthabiti wa bara hilo kwa kutanua ushawishi wao,waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amewaambia marais chungunzima wa bara hilo katika mkutano kwamba China inazidi kuacha alama kila kukicha kupitia ushawishi wake wa kiuchumi unaoongezeka barani Afrika.
Lakini kinachoitia wasiwasi zaidi Marekani kwa mujibu wa waziri wake huyo wa ulinzi ni kile alichokiita ni China kutokuwa muwazi siku zote katika kile inachokifanya.
China imekuwa ikifanya mkutano na viongozi wa bara hilo la Afrika kila baada ya miaka mitatu katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Japokuwa inaonesha waziwazi kwamba kuna ushindani wa kimaslahi baina ya China na Marekani kuelekea bara hili la Afrika,maafisa wa Marekani wamejizuia kuonesha mkutano huu kama ni mapambano ya kuwania ushawishi.