1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatoa ndege mbili za kusafirisha wanajeshi wa Umoja wa Afrika

ELIZABETH KEMUNTO19 Oktoba 2004

Rais wa Marekani George W Bush, ametoa amri kwa waziri wake wa ulinzi, atoe ndege mbili za kijeshi ambazo zitasaidia kuwasafirisha wanajeshi wa Umoja wa Afrika hadi nchini Sudan. Ndege hizo zitatolewa kwa muda wa wiki mbili.

https://p.dw.com/p/CEHV

Inasemekana ya kwamba Marekani inashirikiana na mataifa mengine ya kimataifa kama vile Australia, Ubelgiji, Canada, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza na Umoja wa Ulaya, kusaidia kupanua kikosi cha Umoja wa Afrika, ambacho kinatarajiwa kuwa na wanajeshi elfu tatu na mia tano.

Waziri wa mambo ya nje Collin Powell, anawasiliana na washirika wa Marekani wa kimataifa, na anawashawishi waunge mkono Umoja wa Afrika.

Kikosi cha Umoja wa Afrika kinatarajiwa kusimamia kumalizika kwa vita, na kurudisha hali ya usalama, itakayoruhusu mashirika ya misaada kufika Darfur na kutoa misaada.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na ikulu ya White House, Rais Bush amesema anakubaliana na uongozi wa Rais Obasanjo kama Rais wa Umoja wa Afrika na jinsi anavyokabaliana na mzozo wa Darfur. Taarifa hiyo imeendela kueleza kwamba, Marekani inatoa wito kwa serikali ya Sudan na waasi wa Darfur kumaliza vita na kufanya jitihada za kufikia mapatano.

Wakati huo huo, mkuu wa usalama nchini Sudan Salah Gosh, amesema waasi katika jimbo la Darfur wamerundika silaha katika vijiji vya Darfur, na kuvitumia vijiji hivyo kama vituo vyao vya kijeshi.

Gosh amekiri kwamba serikali ya Sudan ilihami makabila ya kiarabu na silaha, ambazo zilitumiwa kupigana na waasi wa Darfur. Hata hivyo amesema serikali haiwezi kufanya kosa kama hilo tena katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo, kwani tayari kuna hali ya wasiwasi katika mpaka na Eritrea.

Mashambulizi ya vijiji na ndege za kivita, wanajeshi na wanamgambo, yamesababisha watu milioni moja nukta tano kuyahama makazi yao, na kuletea jamii ya kimataifa kushutumu serikali ya Sudan kwa kukosa kumaliza mashambulizi hayo.

Umoja wa Mataifa umetishia kuiwekea Sudan vikwazo, kwa kile ambacho umoja huo umekitaja kuwa ukiukaji mbaya zaidi wa haki za binadamu.

Serikali ya Sudan haijawahi kuzungumzia mashambulzi ya anga katika vijiji vya Darfur, licha ya ushahidi mwingi kuhusu mashambulizi hayo.

Lakini mkuu wa usalama Bwana Gosh, amesema waasi wanashambulia majeshi ya serikali kutoka kwa vijiji, na serikali imelazimika kulipua vijiji hivyo ikitumia mabomu. Gosh amesema serikali itaendelea kushambulia vijiji hivyo kwa sababu vinashambulia wanajeshi wa serikali.

Amesema ni kawaida kwa waasi kuwaambia wakazi wa vijiji watoroke kabla ya kuanza mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa serikali, na ndio sababu watu wengi hawana makao.

Baada ya miaka mingi ya mizozo ya maji na ardhi kati ya makabila ya kiarabu na kiafrika, huko Darfur, waasi walianza vita mwaka jana, wakiilaumu serikali ya Sudan kwa kutojali makabila ya waafrika, pamoja na kutumia wanamgambo wa janjaweed kuchoma na kupora vijiji vyao.

Serikali ya Sudan imekiri kuwapa silaha wapiganaji dhidi ya waasi, lakini imekanusha kuwepo na uhusiano wowote kati yake na wanamgambo wa janjaweed na imewaita wahalifu.

Gosh amesema waasi mara nyingi wanaweka kambi zao karibu na vijiji ambapo kuna maji, na waasi hao wanafanya mashambulizi dhidi ya majeshi ya serikali wakiwa ndani ya vijiji.

Gosh ameongeza kwamba tatizo sio kuwauwa raia bali ni waasi wanawatumia raia kama ngao. Mkuu huyo wa usalama ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kushughulikia mashambulizi katika mji wa Fallujah nchini Irak, ambayo hayatofautishi raia na waasi.

Umoja wa Mataifa unasema watu wapatao elfu sabini wamekufa kutokana na njaa na magonjwa, tangu vita katika eneo la Darufur kuanza.

Bwana Gosh amekiri kwamba haki za binadamu zimekiukwa, na wale ambao wamehusika wataadhibiwa. Ametoa wito kwa kumalizika kwa mashambulizi na kuanzishwa mahakama katika eneo hilo, na kuwapeleka polisi wapate kufanya upelelezi.

Mkuu huyo wa usalama amesema serikali imechoka kuvumilia kuvunjwa kwa makubaliano ya kumaliza vita na waasi huko Darfur, katika wiki chache zilizopita.

Gosh amesema kwamba kutokana na mashambulizi ya waasi, serikali imechukua watu kutoka kwa makabila ya eneo hilo na kuwapa mafunzo ya kijeshi pamoja na silaha. Makabila yaliyopewa silaha ni ya kiarabu ingawa kuna mengine ambayo yalikuwa sio ya kiarabu. Watu hawa waliingizwa katika jeshi ili kupambana na waasi, lakini wengi wao walitoroka na kurudi vijijini wakiwa na silaha walizopewa.