Marekani yaunga mkono viti viwili vya kudumu vya Afrika UN
13 Septemba 2024Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield, anatarajiwa kuutangaza uamuzi huo Alhamisi.
Hatua hiyo inachukuliwa wakati ambapo Marekani inajaribu kurekebisha uhusiano wake na Afrika, ambako wengi hawajafurahishwa na suala la Marekani kuunga mkono vita vya Israel huko Gaza, na kuimarisha uhusiano na mataifa ya Visiwa vya Pasifiki, ikiwa ni muhimu katika kukabiliana na ushawishi wa China unaoongezeka katika eneo hilo.
Soma zaidi: Wito watolewa Afrika kupewa viti vya kudumu UN
Thomas-Greenfield ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa ana matumaini tangazo hilo litasogeza mbele ajenda hiyo kwa njia ambayo wataweza kufikia mageuzi ya Baraza la Usalama wakati fulani, katika siku zijazo, akiielezea kama sehemu ya kumbukumbu itakayoachwa nyuma na Rais wa Marekani, Joe Biden.
Kushinikiza uwepo wa viti viwili vya kudumu kwa mataifa ya Afrika, na kiti kimoja cha kupokezana kwa mataifa ya visiwa vidogo vinavyoendelea, ni mwendelezo wa hatua ya muda mrefu ya Marekani kuunga mkono India, Japan, na Ujerumani kupata pia viti vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kabla ya kutangaza hilo baadae leo katika Baraza la Uhusiano wa Kigeni mjini New York, Thomas-Greenfield alifafanulia Reuters kwamba Marekani haiungi mkono upanuzi wa nchi tano wanachama wa kudumu zenye mamlaka ya kupiga kura ya turufu katika baraza hilo.
Madai ya muda mrefu ya nchi zinazoendelea
Kwa muda mrefu nchi zinazoendelea zimekuwa zikidai kupata viti vya kudumu katika Baraza la Usalama, chombo chenye nguvu zaidi katika Umoja wa Mataifa. Lakini mazungumzo ya miaka mingi kuhusu mageuzi hayajazaa matunda, na haiko wazi ikiwa uungaji mkono wa Marekani unaweza kuchochea hatua hiyo.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina jukumu la kudumisha amani na usalama, na lina mamlaka ya kuweka vikwazo, na marufuku ya silaha na kuidhinisha matumizi ya nguvu.
Akizungumza Jumatano na Reuters, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema anaunga mkono mageuzi katika Baraza la Usalama.
Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Wakati Umoja wa Mataifa ulipoanzishwa mwaka 1945, Baraza la Usalama lilikuwa na wanachama 11.
Mwaka 1965 kulikuwa na wanachama 15, wakiwemo 10 ambao sio wa kudumu, kwani wanachaguliwa kwa kipindi cha miaka miwili miwili, na wanachama watano wa kudumu, wenye mamlaka ya kupiga kura ya turufu.
Nchi wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni Urusi, China, Ufaransa, Marekani na Uingereza.
(Reuters)