Marekani yauonya utawala wa Korea Kaskazini
30 Novemba 2017Marekani imeuonya utawala wa Korea Kaskazini kwamba utaangamizwa iwapo vita vitazuka, kufuatia jaribio la kombora la masafa marefu hapo jana. Akizungumza mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa balozi wa Marekani katika Umoja huo, Nikki Haley, alionya kwamba dikteta wa Korea Kaskazini, Kim Jon Un, alichagua jana kuuleta ulimwengu karibu na vita.
"Hatujawahi kutafuta vita na Korea Kaskazini na hata leo hatuvitaki. Kama vita vitakuja, itakuwa ni kwa sababu ya vitendo vya mara kwa mara vya uchokozi kama ilivyoshuhudiwa jana. Na vita vitakapokuja, utawala wa Korea Kaskazini utaangamizwa kabisa."
Haley alisema Marekani imeitaka China kusitisha kabisa usafirishaji wa mafuta kwa Korea Kaskazini, hatua pekee ambayo taifa hilo jirani na mshirika pekee wa kibiashara na Korea Kaskazini, limekuwa likisita kuichukua.
Naibu balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Wu Haitao, alisema China imewasilisha pendekezo la mpango unaolenga kuizuia Korea Kaskaini kumiliki silaha za nyuklia na wakati huo huo kudumisha amani katika rasi ya Korea. Haitao aidha alisema China inaamini kazi inayofanywa na kamati ya vikwazo ya baraza la usalama sharti ihakikishe eneo la Korea halina silaha za nyuklia, amani na uthabiti vinadumishwa na mdahalo na mazungumzo yanaendelezwe kati ya pande husika kwa lengo la kutafuta suluhisho.
Haitao pia alisema, "Ni msimamo wa China kwamba vikwazo vya baraza la usalama dhidi ya Korea Kaskazini havipaswi kusababisha athari hasi kwa shughuli za utoaji wa huduma za kibinadamu."
Urusi yapinga wito wa Marekani
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia, alisema kwao wao ni bayana kwamba hakuna suluhisho la kijeshi kwa matatizo ya eneo la Korea. Alizitolea mwito pande zote husika ziache kuchochea hali ya wasiwasi inayosababishwa na kauli za vitisho zinatolewa pamoja na majibizano.
"Ni muhimu kuchukua hatua nyuma na kutathmini kwa uangalifu mkubwa athari za kila hatua, kudurusu upya sera ya vitisho vya pamoja kwa sababu sera hii husababisha tu matokeo au malengo ambayo ni kinyume cha yale yanayokusudiwa."
Akizungumza akiwa nchini Belarus, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urisi, Sergei Lavrov, aliupinga wito uliotolewa na Marekani kuitenga Korea Kaskazini.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana jana kufuatia ombi la Marekani, Japan na Korea Kusini kutafakari hatua zinazotakiwa kuchukuliwa baada ya duru tatu za vikwazo vilivyoidhinishwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kushindwa kuishinikiza Korea Kaskazini kubadili msimamo wake.
Balozi wa Ufaransa katika umoja wa Mataifa, Francois Delattre, amesema baraza la usalama linatakiwa kuchukua hatua kwa kuimarisha vikwazo, hatua ambayo yumkini ikajumuisha kuidhinishwa kwa azimio jipya la vikwazo. Naye balozi wa Japan katika umoja huo, Koro Bessho, amesema jumuiya ya kimataifa inatakiwa iendelee kuongeza shinikizo.
Siku ya Jumatano Korea Kaskazini ilifanya jaribio la kombora la tatu la masafa marefu ambalo ilidai lina uwezo wa kupiga eneo lolote la Marekani. Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, alisema jaribio hilo limetimiza lengo la kuwa dola linalomiliki silaha za nyuklia.
Mwandishi:Josephat Charo/afpe/reuters
Mhariri:Yusuf Saumu