1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yazikosoa pande hasimu Sudan Kusini

10 Januari 2014

Marekani imezikosoa pande zote mbili za mzozo wa Sudan Kusini kwa kutokupiga hatua ya maana kwenye mazungumzo ya amani mjini Addis Ababa, Ethiopia huku mapigano yakiendelea na mauaji yakiongezeka.

https://p.dw.com/p/1AoSb
Baadhi ya wajumbe wa mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Baadhi ya wajumbe wa mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini mjini Addis Ababa, Ethiopia.Picha: Reuters

Mshauri wa Usalama wa Rais Barack Obama wa Marekani, Susan Rice, ameelezea namna nchi yake inavyokerwa na vile kiongozi wa waasi, Riek Machar, anavyosisitiza kuachiwa kwa mahabusu kama shari la kuendelea na mazungumzo ya amani.

Lakini kwa upande mwengine, katika taarifa yake ya jana (tarehe 9 Januari), Balozi Rice alisema Marekani pia inafadhaishwa na Rais Salva Kiir kutowaachia mahabusu hao.

Kwa sasa, kikwazo kikuu cha mazungumzo hayo kimekuwa ni madai hayo ya kuachiwa kwa wanasiasa hao 11, ambao waliwekwa kizuizini mara tu machafuko yalipoanza tarehe 15 Disemba.

Rais Kiir amekuwa akisisitiza kwamba washirika hao muhimu wa Machar, anaowatuhumu kujaribu kuipindua serikali yake, hawawezi kuachiwa bila ya kwanza kupitia utaratibu wa kisheria.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Marekani imezitaka pande zote mbili kusaini haraka makubaliano ya kusitisha mapigano, yanayosimamiwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi Afrika ya Mashariki na Pembe ya Afrika (IGAD) mjini Addis Ababa.

Wapatanishi wana matumaini

Hata hivyo, mjini Addis Ababa kwenyewe mpatanishi mkuu wa IGAD, Seyoum Mesfin, amesema ana matumaini aasi na serikali watafikia makubaliano.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amekataa kuwaachia wanasiasa 11 washirika wa Riek Machar.
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amekataa kuwaachia wanasiasa 11 washirika wa Riek Machar.Picha: Reuters

"Ukiniuliza uwezekano wa kusainiwa kwa makubaliano, nitakwambia nina matumaini makubwa.... kwa kuwa hadi sasa tumefikia pakubwa katika kujenga maelewano kati ya pande hizi mbili." Amesema Seyoum.

Mkuu huyo wa upatanishi ameongeza kwamba anatazamia usitishwaji mapigano utatangazwa muda mfupi ujao, ingawa hakueleza muda gani hasa. Kwa sasa, jumuiya ya IGAD inapigania kuzirudisha tena pande mbili kwenye mazungumzo yaliyokuwa yamekwama kwa siku kadhaa sasa.

Mapigano yaendelea

Kauli ya Seyoum inakuja huku kukiwa na taarifa za mapigano mapya na vikosi vya serikali vikikaribia eneo lenye mafuta mengi la Bentu, linaloshikiliwa na waasi. Mapigano makali ya kuwania udhibiti wa mji huo yamepelekea kiasi cha raia 8,000 kukimbilia kwenye jengo la Umoja wa Mataifa kusaka hifadhi.

Wakimbizi wa ndani ya Sudan Kusini, ambao wanalazimika kukimbia makwao kutokana na mapigano.
Wakimbizi wa ndani ya Sudan Kusini, ambao wanalazimika kukimbia makwao kutokana na mapigano.Picha: Reuters

Umoja wa Mataifa umesema ulishakata mawasiliano ya kijeshi na serikali na kwamba uko tayari kukabiliana na yeyote atakayewashambulia raia hao unaowalinda.

Huku idadi ya wanaopoteza maisha na kujeruhiwa ikiongezeka, hospitali katika nchi hiyo changa na masikini zinaonekana kuelemewa na mzigo wa wagonjwa zisizomudu kuwahudumia.

Waziri wa Afya wa Jimbo la Bahr El Ghazal, Tong Deng, asubuhi ya leo (tarehe 8 Januari) alizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi, Kenya, ambako alizungumzia hali mbaya inayolikabili jimbo lake.

"Kama tunavyoona kwenye vita hivi vinavyoendelea Sudan ya Kusini, ni sisi wizara ya afya tunaoshughulikia na madhara ya mgogoro wote, kama vile watu waliopigwa risasi kwenye mapigano, lakini tuna madaktari wachache sana." Alisema Waziri Deng.

Umoja wa Mataifa unakisia kuwa zaidi ya watu 1,000 wameshauwa hadi sasa na wengine zaidi ya 200,000 kugeuzwa wakimbizi wa ndani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/dpa
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman