Marine Le Pen amesema hana ajenda yoyote ya siri kuhusu EU
12 Aprili 2022Kwenye mahojiano na redio ya Ufaransa, France Inter, Marine Le Pen amesema hana ajenda yoyote ya siri kuhusu umoja wa Ulaya.
''Nadhani idadi kubwa ya Wafaransa hawataki tena Umoja wa Ulaya kama ulivyo leo, ambao ni Umoja wa Ulaya unaofanya kazi kwa njia isiyo ya kidemokrasia kabisa, ambao unajiendesha kwa vitisho, kwa usaliti na ambao unatekeleza sera ambazo ni kinyume na maslahi ya wananchi."
Hata hivyo Le Pen ameachana na mipango ya zamani ya kuiondoa Ufaransa kutoka Umoja wa Ulaya, muungano wa Schengen na katika sarafu ya Euro. Lakini, bado ana shaka sana juu ya umoja wa ulaya.
Anasema angeweza kujadili upya makubaliano juu ya eneo la Schengen na kuongeza idadi ya mawakala wa forodha, kuanzisha upya ukaguzi wa bidhaa zinazoingia nchini kutoka mataifa mengine ya umoja wa ulaya. Marine Le pen anasema hatua kama hiyo itakuwa ni kupambana na udanganyifu, lakini wachambuzi wanasema inazua maswali juu ya biashara isiyo na msuguano ndani soko moja la EU.
Soma pia→Le Pen kuchuana na Macron katika duru ya pili ya uchaguzi
Sarkozy kumpigia kura Macron
Hatimaye, Le Pen anatarajia EU kama muungano wa nchi wanachama. Alipoulizwa kama ataiondoa nchi yake katika umoja wa ulaya ikiwa majaribio yake yote ya mageuzi ya muungano huo yatashindwa, Le Pen alijibu ''Hapana hata kidogo.''
Wakati huo huo Rais wa zamani wa Ufaransa wa mrengo wa kulia Nicolas Sarkozy anasema atampigia kura Emmanuel Macron katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais dhidi ya kiongozi wa mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen.
Soma pia→Ufaransa yafanya uchaguzi wa rais
Duru ya pili mnamo wiki mbili
Sarkozy ameandika kwenye ukarasa wake wa Facebook nimemnukuu ''Nitampigia kura Emmanuel Macron kwa sababu ninaamini ana uzoefu unaohitajika katika kukabiliana na mzozo mkubwa wa kimataifa'',mwisho wa kumnukuu.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitahadharisha wafuasi wake kwamba bado wana safari ndefu ya kuibuka na ushindi licha ya kuongoza kwa takribani asilimia 28 katika duru ya kwanza ya uchaguzi uliofanyika, Jumapili, dhidi ya mpinzani wake mkuu, Marine Le Pen, aliyepata takribani asilimia 23. Kampeni za duru ya pili zilianza jana Jumatatu kabla ya uchaguzi hapo April 24.