1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashaka ya Kimbunga Hidaya kwa Wakenya

4 Mei 2024

Mamlaka ya hali ya hewa nchini Kenya imewataka wakaazi wa pwani ya nchi hiyo kuwa katika hali ya tahadhari, wakati eneo hilo likitarajiwa kukumbwa na kimbunga Hidaya.

https://p.dw.com/p/4fUoe
Mafuriko ya nchini Kenya
Kikosi cha zimamoto kinaelekeza katika barabara kuu ya Athi River-Namanga ambayo iliathirika baada ya mto kuvunja kingo zake kufuatia mvua kubwa inayonyesha katika manispaa ya Kitengela kaunti ya Kajiado.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Hadi usiku wa kuamkia leo maisha yameendelea kama kawaida, japo ilikuwa dhahiri kuwa hali ya upepo na mawimbi imebadilika. Upepo mkali umekuwa ukivuma katika maeneo mbalimbali ya Pwani ya Kenya hasa mjini Mombasa, wataalam wa hali ya hewa wanasema kuwa hii ni moja ya dalili ya Kimbunga Hidaya kinachotarajiwa kushuhudiwa wakati wowote katika maeneo ya bahari ya Hindi.

Shughuli za uvuvi baharini, uogeleaji na usafiri zimepigwa marufuku mjini Mombasa kwa muda wa siku tatu,watalii pia wamekatazwa kutembea kwenye fuo za bahari kwa usalama wao.

Onyo kali la polisi katika eneo la Pwani

Kamanda wa Polisi eneo la Nyali pwani ya Kenya Daniel Mumasaba.anasema "Mnaona namna bahari ilivyo, imechafuka vilivyo na tumeonywa na vyombo vya habari kwamba bahari ni mbaya na tunashuhudia na macho sisi wenyewe, natoa amri, kuanzia muda huu hakuna mtu anatakiwa kwenda baharini mpaka tarehe 5. Hakuna boti inaruhusiwa kuingia kwa maji mpaka hii bahari itulie”  Alisema Kamanda Mumasaba.

Mumasaba amesisitiza kuwa kamati ya usalama ikishirikiana na mamlaka ya usafiri wa baharini nchini Kenya (Kenya Maritime Authority) inaendelea kushika doria ufuoni hadi pale serikali itatangaza kimbunga hicho kimeshapita,

Hofu ya wavuvi na wafanyabiasahara kwa kimbunga Hidaya

Mafutiko nchini Kenya
Wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu wa Kenya na watu waliojitolea kufanya kazi za utafutaji na uokoaji, karibu na nyumba zilizokumbwa na mafuriko katika kaunti ya Machakos, Kenya, Aprili 22, 2024Picha: Brian Inganga/AP/picture allinace

Aidha baadhi ya wavuvi akiwemo Frank Nyiro na Ali Mussa na wafanyibiashara wa ufuoni Mombasa wameeleza wasiwasi wao wa kupata hasara wanapotii amri iliyotolewa." Kiukweli siku ya leo ina mabadiliko makubwa sana hasa kwa upande wa hizi ofisi zetu ambazo ni bahari yetu upepo umebadilika si kawaida tumekubali matangazo ya serikali cha kufanya ni kutulia  lakini imetuathiri sana kibiashara, hatuna kazi mpaka hizo siku tatu ziishe, imetutatiza kiasi". Alisema Nyiro.

Lakini Ali Mussa nae aliongeza kwa kusema " Kimbunga cha hidaya kishatufikia dalili twaziona, kuna upepo mkali, mkali sana tu, halafu mara stima zinakata mara zinarudi yaani, kiufupi kishatufikia na sasa watu wa kurauka kama sisi ambao lazima tutoke ndio tupate riziki ni mtihani lakini hatuna budi lazima tuvuke pale feri lazima tupande tuvuke pale feri zahma tunalo lakini mungu tu atusaidie.”

Maafisa wa Shirika la msalaba mwekundu mjini Mombasa wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wenyeji mitaani na pia kwenye redio, kuwaelimisha kuhusu athari za kimbunga hicho,mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha na jinsi ya kuchukua tahadhari ili kujiepusha na maafa ya mafuriko.

Maeneo ya tahadhari kwa kimbunga

Kimbunga Hidaya kinatarajiwa kuvuma katika Bahari ya Hindi na kusababisha upepo mkali, mvua na mawimbi makubwa.Kaunti zilizotajwa kuwa na hatari ya kuathiriwa na mafuriko kutokana na utabiri wa hali ya hewa pwani ya Kenya ni pamoja na Kilifi, Taita Taveta, Tana River, Kwale na Lamu. Kaunti hizo za pwani bado hazijaathirika na mvua kubwa inayoendelea kunyesha sehemu zingine nchini lakini serikali ina wasiwasi kutakuwa na mafuriko.

Soma zaidi:Kenya yaahirisha tena kufungua shule wakati ikiajiandaa kukabiliana na kimbunga Hidaya

Aidha wakaazi wa kaunti ya Lamu wanaoishi maeneo ya visiwani, kama Kisiwa cha Pate ,kisiwa cha Ndhau na kisiwa cha Kiwayu, hawataruhusiwa kusafiri baharini kuanzia leo jioni hadi siku ya jumanne wiki ijayo kufuatia tahadhari ya kimbunga Hidaya.

DW Mombasa