Mashambulizi dhidi ya Gaddafi yazidishwa
20 Machi 2011Kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani, Michael Mullen, amesema majeshi ya kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, sasa hayasongi tena mbele kuelekea mjini Benghazi.
Mullen amesema kuwa sehemu ya kwanza ya operesheni hiyo ya kimataifa kulazimisha upigaji marufuku urukaji ndege katika anga ya Libya imekua ya mafanikio.
Kwa upande mwengine, mapema leo (20.03.2011), Shirika la Utangazaji la CBS News liliripoti kwamba ndege tatu za kivita za Marekani aina ya B-2 zilidondosha mabomu 40 katika uwanja mkuu wa ndege za jeshi la anga la Libya, katika jaribio la kuziharibu ndege zake za kivita.
Taarifa nyengine za jeshi la Marekani zinasema kwamba, magari kadhaa ya kijeshi ya Gaddafi yameharibiwa. Kiasi ya ndege 19 za kijeshi za Marekani zilishiriki katika mashambulizi ya pamoja na Ufaranasa na Uingereza dhidi ya ngome za Gaddafi hivi leo (20.03.2011).
Duru za huduma ya afya mjini Tripoli zinasema idadi ya Walibya waliouawa katika hujuma hizo imepanda kutoka 48 hadi 64 baada ya baadhi ya majeruhi kufariki dunia.
Kwa upande wake, Gaddafi amesema kwamba sasa Walibya wote wamepewa silaha na kwamba wanajiandaa kwa vita virefu alivyoviita "vya kishujaa".
Katika hotuba yake iliyotangazwa na vyombo vya habari vya serikali, Gaddafi amesema Walibya watapigania nchi yao na kutetea utu na heshima yao, akizitaja nchi za magharibi kuwa ni wahalifu.
Kwa upande wao, waasi wameonya kwamba majeshi ya Gaddafi yanaweza kutumia silaha za kemikali dhidi ya wakaazi wa mji wa Benghazi.
Mjini Berlin, Waziri wa Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle ameyapuuza madai kwamba Ujerumani inatengwa kimataifa kwa kukataa kujiunga na washirika wake wa Shirika la Kujihami la Magharibi (NATO) kuihujumu Libya.
Akiulizwa ni nchi gani za Umoja wa Ulaya zinakubaliana na uamuzi wa Ujerumani, Westerwelle alisema ni Poland. Uamuzi wa serikali ya Ujerumani kutoshiriki katika hatua ya kijeshi nchini Libya umezusha shutuma kali hapa nchini.
Gazeti moja liliilaumu serikali kwa kile ilichokiita "kuwa upande wa madikteta kuliko washirika wake muhimu wa NATO".
Westerwelle amesema Ujerumani ina wanajeshi 7,000 katika harakati za kusimamia amani nchi za nje, wakiwemo 5,000 nchini Afghanistan. Kwa hivyo inatimiza wajibu wake kimataifa.
Wakati huo huo, Urusi imetangaza itawahamisha raia wake na wafanyakazi wa ubalozi wake mjini Tripoli. Zoezi hilo litafanyika kwa kutumia magari kupitia nchi jirani ya Tunisia.
Hapo jana (19.03.2011), Urusi ilisema inasikitishwa kuona hatua ya kujiingiza nchini Libya imepitishwa bila kipimo. Pia vyombo vya habari nchini Urusi vimeinukuu duru moja ya Ikulu ya nchi hiyo ikisema kwamba, balozi wake mjini Tripoli amefukuzwa kazi, bila ya kueleza sababu hasa ya hatua hiyo.
Urusi na China, ambazo sawa na Marekani, Ufaransa na Uingereza zina kura ya turufu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zilijiunga na Ujerumani, India na Brazil, kujizuwia kupiga kura juu ya azimio lililopitishwa na Baraza hilo kufungua njia ya kuchukuliwa hatua za kijeshi dhidi ya Gaddafi.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/AFP/Reuters
Mhariri: Mohamed Dahman