1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi Syria yasababisha raia kushindwa kupumua

5 Februari 2018

Raia kadhaa wa Syria wanatibiwa baada ya kushindwa kupumua kutokana na mashambulizi ya ndege yaliyofanywa na serikali kwenye mji wa Saraqeb.

https://p.dw.com/p/2s84b
Chemiewaffen Chlorin Gas
Picha: picture alliance/AA/A.Dagul

Shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London, Uingereza limesema raia watano wanapatiwa matibabu kutokana na kukosa pumzi na kushindwa kupumua baada ya serikali ya Syria kutumia silaha za sumu katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi kwenye mji wa Saraqeb uliopo kaskazini magharibi mwa Syria.

Duru za kitabibu zimeeleza kuwa wagonjwa wengine 11 walikuwa wakitibiwa kutokana na gesi yenye sumu ya Chlorine, iliyotumika katika shambulizi hilo. Shambulizi hilo limefanyika siku chache baada ya Marekani kuishutumu serikali ya Syria kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya vikosi vya waasi karibu na mji mkuu, Damascus.

Hata hivyo serikali ya Syria imekanusha madai hayo ikiyaita kuwa ni ''uongo''. Siku ya Ijumaa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis aliwaambia waandishi habari kwamba serikali yake ina wasiwasi gesi ya sarin huenda ikawa imetumika hivi karibuni nchini Syria, ikizinukuu taarifa za mashirika yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na makundi ya waasi.

Marekani haina ushahidi

Hata hivyo, Mattis alisema hana ushahidi kuhusu madai hayo. Mwezi uliopita watu 21 walitibiwa kutokana na matatizo ya kupumua baada ya roketi kurushwa katika ngome ya waasi Mashariki mwa Ghouta, nje kidogo ya Damascus.

Shirika hilo limesema raia wengine 10 wameuawa katika jimbo la Idlib baada ya helikopta kushambulia maeneo kadhaa, huku watu watano wakiwa na matatizo ya kupumua, kutokana na taarifa kwamba gesi ya sumu ilitumika. Raia wengine wanne wameuawa na majeshi ya serikali katika maeneo ya Maaret al Numan na Maasarin. Mkurugenzi wa vikosi vya ulinzi wa raia, Abu Hamdo amesema ndege zinazoaminika kuwa za Urusi zilishambulia hospitali ya Maaret al Numan na kusababisha uharibifu mkubwa.

Syrien Krieg Zerstörung
Mji wa Saraqeb, SyriaPicha: Getty Images

''Ndege zimeanzisha mashambulizi makali na kuharibu jengo la ghorofa saba na jingine la ghorofa nne. Tumepata jumla ya miili sita na mtoto mmoja amejeruhiwa,'' alisema Hamdo.

Wakaazi wa Afrin waandamana

Wakati huo huo, mashirika ya misaada yamezionya nchi zinazowahifadhi wakimbizi wa Syria kutowalazimisha kurejea nyumbani au kujadiliana hatua kama hizo. Ripoti iliyotolewa na mashirika kadhaa ya kibinaadamu imeelezea kwamba maelfu ya wakimbizi wako katika hatari ya kurejeshwa Syria mwaka huu, licha ya kuendelea kwa ghasia na mashambulizi yanayohatarisha maisha ya raia.

Ama kwa upande mwingine maelfu ya watu wameandamana jana katika mji wa Afrin, Syria wakiyataka mataifa yenye nguvu duniani kuingilia kati na kusaidia kusimamisha mashambulizi yanayofanywa na majeshi ya Uturuki dhidi ya Wakurdi na wameishutumu Urusi kwa kuhusika na mauaji dhidi ya raia katika eneo hilo.

Januari 20, Uturuki na waasi washirika wake walianzisha operesheni dhidi ya kundi la wanamgambo wa Kikurdi nchini Syria, YPG, ambalo Uturuki imeliorodhesha kama kundi la kigaidi. Uongozi wa eneo hilo umezitaka Marekani, Umoja wa Ulaya, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na majeshi yanayoongozwa na Marekani kuuzuia haraka uchokozi wa Uturuki.

Hayo yanajiri wakati leo Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kukutana na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, ambapo pamoja na mambo mengine watajadiliana kuhusu Syria na mzozo wa wakimbizi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, AP
Mhariri: Iddi Ssessanga