1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya angani yawaua wapiganaji 12 Syria

Caro Robi
24 Mei 2018

Shambulizii lililolenga maeneo ya kijeshi ya Syria mashariki mwa nchi hiyo  yamewaua takriban wapiganaji 12 wanaouunga mkono utawala wa Syria usiku wa kuamkia leo. 

https://p.dw.com/p/2yEjU
Flugzeugträger USS Eisenhower
Picha: picture-alliance/dpa/Seaman C.A. Michaels

Shirika la kutetea haki za binadamu Syria lenye makao yake Uingereza limesema mashambulizi hayo yamefanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani katika eneo la kusini mwa Albu Kamal ambalo mara kwa mara limeshuhudia mashambulizi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la Dola la Kiislamu IS.

Mkuu wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu Rami Abdel Rahman amesema magari matatu pia yaliharibiwa katika mashambulizi hayo yaliyosababisha vifo vya wapiganaji 12 ambao si raia wa Syria. Hata hivyo Abdel Rahman hakutoa maelezo zaidi kuhusu uraia wa wahanga hao.

Jeshi la Marekani limekanusha kuhusika na shambulizi hilo. Msemaji wa kamanda wa jeshi la Marekani Kapteni Bill Urban amesema hawajafanya operesheni yoyote ya kijeshi dhidi ya majeshi ya Syria wala wapiganaji watiifu kwao na wala hawana ripoti za kuthibitisha kutokea kwa mashambulizi.

IS bado yadhibiti maeneo kadhaa Syria

Dola la Kiislamu IS limepoteza sehemu kubwa ya ngome zake nchini Syria tangu mwaka jana lakini bado linaendelea kudhibiti  maeneo kadhaa ya jangwani na wanamgambo hao wa IS wamekuwa wakiwashambulia wanajeshi wa serikali na wapiganaji wanaowaunga mkono katika kipindi cha majuma ya hivi karibuni.

Syrien Kämpfe in der Nähe von Albu Kamal gegen den IS
Majeshi ya Syria yakiwa katika mji wa Albu KamalPicha: Getty Images/AFP/STRINGER

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani pia hivi karibuni umeanza tena kampeini dhidi ya kundi hilo la kijihadi nchini Syria.

Shirika la habari la Syria SANA limeripoti kuwa vituo vya kijeshi vilivyoko kati ya eneo la Albu Kamal na Humeima vimeshambuliwa mapema leo alfajiri na kusababisha maafa katika vituo hivyo. Mashambulizi hayo yanakuja saa 24 tu baada ya IS kufanya pia mashambulizi katika eneo hilo.

Maeneo ya Abu Kamal na Humeima yako mashariki mwa Syria katika jimbo la Deir Ezzor ambako majeshi ya Syria yanayoungwa mkono na Urusi na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani yamekuwa yakipambana na kundi la IS. Wapiganaji wa Kishia kutoka Iraq pia wanapigana katika eneo hilo kwa ushirikiano na majeshi ya Syria.

Haijabainika kama mashambulizi hayo ya angani yalikuwa yanawalenga wanamgambo au yaliwashambulia wapiganaji watiifu kwa serikali kimakosa.

Hayo yanakuja huku leo Rais wa Urusi Vladimir Putin akikutana na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron mjini Moscow kwa mazungumzo, miongoni mwa ajenda kuu ya mazungumzo yao  ikiwa mzozo huo wa Syria ambao umesababisha vifo vya maelfu kwa maelfu ya watu, kuwaacha mamilioni bila ya makazi nchini humo na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi katika kipindi cha zaidi ya miaka saba sasa.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu