Wizara ya Afya Gaza: Mashambulizi ya Israel yauwa 70
25 Desemba 2023Msemaji wa wizara hiyo, amesema familia kadhaa katika eneo la Al-Maghazi ziliathiriwa na mashambulizi hayo.
Shirika la habari la Ujerumani, DPA, halikuweza kuthibitisha taarifa hizo kwa uhuru. Msemaji wa jeshi la Israeli amesema ripoti hizo zinachunguzwa.
Wanajeshi wa Israel wamekuwa wakifanya mashambulizi katika Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7, baada ya kundi la wanamgambo la Hamas na makundi mengine yenye itikadi kali ya Palestina, kufanya mashambulizi dhidi ya Israel, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na zaidi ya 240 kushikwa mateka.
Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya ni miongoni mwa nchi ambazo zimeliorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.
Kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza, zaidi ya watu 20,258 wameshauawa katika Ukanda huo tangu mwanzo wa vita hivyo na 53,688 wamejeruhiwa, hasa raia.