Machafuko yatokea Gaza
11 Oktoba 2015Nur Hassan, mwenye umri wa miaka 30 na mwanawe wa kike Rahaf Hassan mwenye umri wa miaka 2, wameuwawa wakati nyumba yao kaskazini ya Ukanda wa Gaza , katika eneo la Zeitun ilivunjwa katika shambulio hilo la Israel, wamesema wafanyakazi wa hospitali, ambapo watu wengine watatu bado wamenaswa katika kifusi cha nyumba hiyo.
Israel imesema mashambulizi yake yamelenga "maeneo mawili ya kutengenezea silaha ya Hamas" kujibu maroketi mawili yaliyorushwa dhidi ya Israel siku ya Jumamosi, pamoja na idadi kadhaa ya majaribio yaliyofanywa na Wapalestina kujaribu kwa nguvu kuingia Israel kutokea Gaza.
Moja kati ya maroketi hayo yaliangukia katika maeneo ya wazi kusini mwa Israel na mengine yaliharibiwa hewani kabla ya kufika yalikokusudiwa, wakati Wapalestina tisa wameuwawa katika mapambano ya mpakani na wanajeshi wa Israel.
Jaribio la kuleta utulivu lashindwa
Wakati Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Rais Mahmoud Abbas wakijaribu kuepusha hali mbaya zaidi, vijana wa Kipalestina ambao wanakosa uvumilivu wamekaidi juhudi za kurejesha utulivu na wimbi la kuchomwa visu limesababisha hofu nchini Israel.
Ukanda wa Gaza umekuwa kwa kiasi kikubwa tulivu baada ya ghasia za wiki nzima kwingineko, lakini mapambano ya hivi karibuni, maroketi na mashambulizi ya anga yanaongeza hofu kwamba vuguvugu la mapambano la Wapalestina, ama Intifadha, linaweza kuzuka.
Mapambano ya mpakani siku ya Ijumaa yamekuja wakati kiongozi wa chama cha Hamas katika ukanda wa Gaza, Ismail Haniyah, ameziita ghasia hizo kwa jumla intifada na kuhimiza ghasia zaidi.
Viongozi watupiana lawama
Hamas ambayo inatawala Gaza imeendelea kutofautiana kwa kiasi kikubwa na chama cha Rais Abbas, Fatah, kinachotawala katika ukingo wa Magharibi. Abbas pamoja na Netanyahu wakati huo huo wamezungumza na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, John Kerry, kila mmoja akimlaumu mwenzake kwa kuzusha hali hiyo kwa upande mwingine.
Netanyahu amesema amemwambia Kerry anatarajia mamlaka ya Palestina kuacha "uchochezi wake usio na maana ambao unasababisha wimbi la hivi sasa la ugaidi".
Na Abbas amesema amerudia matakwa yake kwa ya maafisa wa Israel kuacha kutoa ulinzi kwa "uchokozi wa walowezi wa Kiyahudi, unaofanywa chini ya ulinzi wa jeshi".
Kerry amekubaliana na "wasiwasi wake mkubwa" kuhusiana na ghasia hizo katika mazungumzo tofauti na viongozi hao wawili, ofisi yake imesema katika taarifa, na "kusisitiza umuhimu wa kurejea katika hali ya kawaida kwa maneno na vitendo katika eneo la al-Haram al-Sharif ama Temple Mount na kuzuwia maneno ya uchochezi na hatua ambazo zitaongeza hali ya wasi wasi."
Ghasia zimelitikisa eneo lililochukuliwa kimabavu na Israel la Jerusalem mashariki na linalokaliwa kimabavu la Ukingo wa Magharibi, wakati Wapalestina wakirusha mawe na mabomu ya moto dhidi ya majeshi ya usalama ya Israel, ambayo yamejibu kwa kufyatua risasi za moto, risasi za mipira, mabomu ya kutoa machozi na mabomu ya kutishia.
Mapambano yaliitikisa miji ya Ukingo wa Magharibi ya Ramallah na Bethlehem siku ya Jumamosi.
Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef